Habari Mseto

Kizimbani kwa kuiba chupi na sidiria za bosi wake

April 30th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 22, Jumatatu alishtakiwa kwa kuiba nguo za ndani za mwajiri wake mtaani Kangemi, Nairobi.

Bi Bibiane Lihavi alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera Barbara Ojoo akikabiliwa na shtaka la kuiba mali ya mwajiri wake ya thamani ya Sh100,000 zikiwemo nguo za ndani, sindiria, mavazi na simu.

Ilidaiwa kwamba alitenda kosa hilo Aprili 29 katika eneo la Thiongo, Kangemi akiwa mjakazi wa Bi Pauline Wanjiku Wachira.

Bi Lihavi alikanusha shtaka akisema alichopata kwa mlalamishi ni simu pekee. “ Ni yeye aliyenipatia simu hiyo kwa sababu ya kutia bidii kazini. Haya mengine ni ya uongo, ninakataa shtaka,” alisema.

Mahakama iliambiwa kwamba aliiba mali hiyo nyumbani kwa Bi Wanjiku.

Alikiri kwamba alikuwa mfanyakazi wa nyumbani wa mlalamishi.

“Ni kweli nilikuwa nikimfanyia kazi lakini mimi sikuiba mali yake inavyodaiwa,” alisema.

Upande wa mashtaka haukupinga ombi lake la dhamana na Bi Ojoo akamwachilia kwa dhamana ya Sh50,000 na mdhamini wa kiasi sawa hadi Julai 8 mwaka huu kesi itakaposikilizwa.