Habari Mseto

Kizimbani kwa kuiba hela kwa M-Pesa ya mwendazake

August 14th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYAKAZI wa kampuni kubwa zaidi ya mawasiliano Afrika Mashariki, Safaricom alishtakiwa kwa kuiba pesa za mtu aliyekufa kutoka kwa akaunti yake ya M-pesa..

Peter Odhiambo Ochieng alikana aliiba pesa kutoka kwa simu ya marehemu Janet Khaniri. Alikanusha mashtaka mawili na kuomba mahakama imwachilie kwa dhamana.

Mahakama ilifahamishwa mnamo Julai 26 mwaka huu, Odhiambo alimwibia marehemu Janet Sh45,000.

Hakimu mwandamizi Martha Mutuku alifahamishwa kuwa Janet alikuwa ameolewa na Wilson Karani Khaniri.

Kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda alieleza mahakama kwamba mshtakiwa anakabiliwa na kesi nyingine sawa na hilo.

“Mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mengine sawa na hayo. Naomba mahakama itilie maanani kuwa mshtakiwa amekuwa na mazoea ya kuwaibia wafu pesa kutoka kwa akaunti zao za Mpesa,” alisema Bw Gikunda.

Alidaiwa aliiba pesa hizo kutoka kwa simu ya Janet nambari 0722235715.