Habari Mseto

Kizimbani kwa kuiba vifaa vya kupima HIV

July 18th, 2018 1 min read

Na NDUNGU GICHANE

WAHUDUMU watatu wa hospitali ya Murang’a Jumanne walishtakiwa mahakamani kwa kuiba vifaa vya kupima maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ukimwi vyenye thamani ya Sh3 milioni.

Sophia Kinya Nteere, William Muhara Wambugu na James Wairiuko Kamindo na wengine ambao hawakuwa mahakamani walishtakiwa kwamba kati ya Mei 16 na Julai 13 waliiba vifaa 32,400 vya kupima maambukizi hayo vinavyomilikiwa na serikali ya kaunti ya Murang’a.

Watatu hao waliofikishwa mbele ya Hakimu mwandamizi wa mahakama ya Murang’a Antony Mwichigi hata hivyo walikanusha mashtaka dhidi yao na wakaachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 na bondi ya Sh1 milioni kila moja.

Hakimu huyo alisema kwamba kesi dhidi ya watatu hao itendelea Agosti 2.

Washukiwa hao walikuwa miongoni mwa washukiwa watano ambao tayari wamerekodi taarifa katika ofisi ya idara ya uchunguzi wa kihalifu siku mbili zilizopita baada ya wizi huo kugunduliwa siku ya Ijumaa wiki jana.

Kulingana na afisa mkuu wa afya hospitalini humo Kanyi Gitau, thamani ya vifaa hivyo vyote ni Sh5milioni.

Mnamo Jumamosi, DCIO wa Murang’a Kaskazini Japheth Maingi aliahidi kwamba pindi tu uchunguzi utakapokamilika, watakaopatikana na hatia watafikishwa mahakamani.

Wizi huo pia ulihusisha wanafunzi wawili kutoka Taasisi ya mafunzo ya kimatibabu ambao walikuwa wakishiriki mafunzo ya nyanjani, wafanyakazi wawili wa kawaida na wahudumu wanne.

Bw Gitau alidai kwamba waligundua wizi huo walipotaka kuisadia wahudumu wa afya kutoka serikali ya kaunti jirani ya Kirinyaga na vifaa hivyo lakini wapata havipo mahali vinahifadhiwa ndipo wakapiga ripoti kwa polisi.