Habari MsetoSiasa

Kizimbani kwa kujifanya Duale

May 23rd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME aliyejifanya kuwa Kiongozi wa Walio Wengi Bungeni Aden Duale Alhamisi alifikishwa mahakamani.

Bw James Oire Ombui alikabiliwa na mashtaka mawili ya kujifanya kuwa Mbunge wa Garissa Mjini Bw Duale, na pia kujitambulisha kwa watu mbalimbali kuwa msaidizi wa kinara huyu wa chama cha Jubilee bungeni.

Bw Ombui alishtakiwa alijifanya kuwa Bw Duale mnamo Aprili 15 na 16,2019 jijini Nairobi.

Bw Ombui alikanusha mashtaka hayo na kumuomba hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku amwachilie kwa dhamana.

“Naomba hii mahakama imwachilie kwa dhamana mshtakiwa,” wakili Onsongo Morara alimsihi hakimu.

“Mshtakiwa alikuwa ameachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 na kuamriwa afike kortini kujibu mashtaka na alitii. Naomba hii mahakama imwachilie kwa dhamana sawa na hiyo kwa vile ameonyesha utiifu,” Bw Morara alisema.

Kiongozi wa mashtaka Bi Pamellah Avedi hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Hakimu alimwamuru mshtakiwa alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh50,000 na kutenga kesi hiyo itajwe baada ya wiki mbili.