Habari Mseto

Kizimbani kwa kupokea Sh200,000 ili ampe mwanafunzi nafasi Kenya High

February 7th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa ulaghai ameshtakiwa  kwa kupokea Sh200,000 kutoka kwa mzazi aliyetaka bintiye apewe nafasi katika kidato cha kwanza shule ya upili ya Kenya High.

Bi Lilian Wangui Odwoma alikanusha mashtaka manne mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Alidaiwa kuwa mnamo Desemba 10, 2018 alipokea kitita cha Sh200,000 kutoka kwa Bi Monica Wairimu Boro akijifanya alikuwa na uwezo wa kumsaidia kupata nafasi ya kidato cha kwanza katika shule upili ya Kenya High.

Mshtakiwa alidaiwa alighushi barua ya kumwalika Bi Faith Watetu Mugambi kujiunga na shule hiyo yenye fahari kuu.

Bi Faith Watetu Mugambi alikuwa amezoa alama 343 katika mtihani wa darasa la nane.

Mshtakiwa alikabiliwa na shtaka la kujitengenezea muhuri wa shule ya upili ya Kenya High.

Pia alishtakiwa alimpelekea Bi Wairimu barua hiyo akidai ilikuwa halisi ya kumwalika Faith ajiunge na kidato cha kwanza katika shule hiyo iliyo na fahari kuu.

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana na kesi kuorodheshwa kusikizwa Februari 25, 2019