Michezo

Kizungumkuti cha Shakava, Otieno na Abuya kurejea Zambia kuvalia jezi za Nkana FC

July 13th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NKANA FC ambao ni mabingwa mara 12 wa Ligi Kuu ya Zambia (ZSL), watakosa huduma za Wakenya Harun Shakava, Duncan Otieno na Duke Abuya kipute hicho kitakaporejelewa wikendi hii.

Wanasoka hao watatu, akiwemo beki Musa Mohammed, walirejea humu nchini mnamo Machi 2020 baada ya janga la corona kusababisha kusitishwa kwa kampeni za ZSL zikiwa zimesalia mechi 10 zaidi msimu huu.

Musa alikuwa pia akivalia jezi za Nkana kabla ya kulipuka kwa corona. Mkataba wake na miamba hao ulitamatika rasmi mwezi uliopita na hajapokezwa kandarasi nyingine hadi kufikia sasa.

Kwa mujibu wa Shakava, marufuku yanayozuia usafiri wa kimataifa kuelekea jijini Lusaka hadi mwanzoni mwa Agosti, utawaweka katika ulazima wa kukosa sehemu ya kampeni zilizosalia za waajiri wao.

Difenda huyo wa Harambee Stars amefichua kwamba hakuna mipangilio yoyote ambayo imewekwa na Nkana ili kuwezesha kusafiri kwao, na hilo linazima kabisa matumaini yao ya kujiunga na wenzao waliorejea kambini wiki mbili zilizopita mwa minajili ya mechi zilizosalia na vipute vya msimu ujao wa 2020-21.

Hadi kivumbi cha ZSL kilipositishwa, Nkana ambao wana makao yao mjini Kitwe, walikuwa wakishikilia nafasi ya nne kwa alama 43, tatu pekee nyuma ya viongozi wa jedwali, Forest Rangers wanaompa hifadhi nahodha wa zamani wa Sofapaka, Mathias Kigonya.

Shakava ambaye ni kapteni wa zamani wa Gor Mahia, angali nyumbani kwao Kakamega. Amefichua kwamba Nkana waliwahi kuwapendekezea kusafiri hadi Tanzania kisha kuunganisha safari yao hadi Zambia ila jaribio lao la kuingia ndani ya mpaka wa Tanzania kinyume na kanuni zinazodhibiti maambukizi ya corona likatibuka.

“Tutakosa kinyang’anyiro cha ZSL kinachorejelewa Jumamosi hii. Bado hakuna ndege za abiria zinazoruhusiwa kuelekea Zambia na juhudi zetu za kuingia Tanzania ili kuunganisha safari zimeambulia patupu mara kadhaa. Timu ilianza mazoezi majuma mawili yaliyopita na tuna hofu huenda tukakosa mechi zote za Nkana zilizosalia msimu huu,” akasema.

Kutokana na suitafahamu hiyo, Shakava amekiri kwamba AFC Leopards, Wazito FC na vikosi vingine viwili vya ughaibuni, vimejaribu sana kumfikia kupitia kwa wakala wake kuhusu uwezekano wa kumsajili.

“Nazidi kupokea ofa mbalimbali ambazo ninazitathmini kwa pamoja na wakala wangu. Iwapo kurejea Nkana kutazingirwa na kizungumkuti kikubwa, basi sitakuwa na budi ila kutamatisha mkataba wangu unaokatika mnamo Julai 2021 na kutafuta kikosi kipya,” akaongeza.