Michezo

Kizungumkuti cha wawakilishi wa EPL katika UEFA

June 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MATUMAINI ya Manchester City, Chelsea, Manchester United na Wolves katika soka ya bara Ulaya (Uefa na Europa League) yametiwa kwenye giza totoro baada ya serikali ya Uingereza kutangaza kanuni mpya za kuzingatiwa na wageni katika jitihada za kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Wageni wote watakaokuwa wakiingia nchini Uingereza kuanzia Juni 8, 2020 watakuwa wakitiwa kwenye karantini ya lazima kwa jumla ya siku 14.

Hatua hiyo mpya haikusaza ulingo wa spoti; jambo ambalo kwa sasa lina kila sababu ya kuwaumiza vichwa wawakilishi wa Uingereza katika soka ya bara Ulaya muhula huu.

Awali, wasimamizi wa klabu za Man-City, Man-United, Chelsea na Wolves walikuwa wamewasilisha ombi kwa Katibu Mkuu wa Masuala ya Utamaduni nchini Uingereza, Oliver Dowden, kukubalia kanuni hiyo mpya ya usafiri kutoathiri vikosi vya kigeni ambavyo vingefika Uingereza kwa mechi za UEFA na Europa League.

Hata hivyo, Dowden alishindwa kusadikisha mawaziri kuhusiana na misingi ya pendekezo hilo katika kikao kilichowajumusha maafisa wa serikali na wataalamu wa afya. Watu wa pekee ambao hawatadhibitiwa na kanuni hiyo ni maafisa wa ngazi za juu zaidi katika serikali za mataifa ya kigeni, marubani wa ndege za mizigo na maafisa wa afya.

Ina maana kwamba iwapo Real Madrid watatua nchini Uingereza kwa marudiano ya mechi ya hatua ya 16-bora ya UEFA dhidi ya Man-City, miamba hao wa Uhispania watalazimika kusubiri jijini Manchester kwa wiki mbili zaidi ili kuvaana na wenyeji wao.

Kwa upande wao, Chelsea pia wanatarajiwa kutua Ujerumani kuvaana na Bayern Munich kwenye marudiano ya UEFA. Hilo litawaweka masogora hao wa kocha Frank Lampard katika ulazima wa kukaa karantini kwa siku 14 pindi watakaporejea Uingereza.

Man-United wanapigiwa upatu wa kutwaa ubingwa wa Europa League baada ya kupiga LASK 5-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora uliosakatiwa nchini Austria. Mkondo wa pili utachezewa ugani Old Trafford huku Wolves wanaotazamiwa kuchuana na Rangers ya Scotland wakikabiliwa na kizungumkuti sawa na hicho.

Ilivyo, soka ya EPL inatazamiwa kuanza upya mnamo Juni 12, 2020 wakati sawa na ule ambao vinara wa Uefa wanalenga pia kurejelea kampeni za soka ya bara Ulaya kwa matarajio ya kukamilisha vipute hivyo kufikia mwisho wa Agosti 2020.

Kwa mujibu wa Aleksander Ceferin ambaye ni Rais wa Uefa, robo-fainali na nusu-fainali za vipute vya UEFA na Europa League zitahusisha michuano ya mikondo miwili; yaani mechi zitasakatwa na kila kikosi nyumbani na ugenini.

Iwapo mtazamo wa Ceferin utakumbatiwa na wadau wengine katika kikao kijacho, basi huenda fainali ya UEFA ikaandaliwa jijini Istanbul, Uturuki mnamo Agosti 29, 2020 siku tatu baada ya kutandazwa kwa fainali ya Europa League jijini Gdansk, Poland.