Klabu 12 kunogesha Jamhuri Cup Mombasa

Klabu 12 kunogesha Jamhuri Cup Mombasa

ABDULRAHMAN SHERIFF na JOHN KIMWERE

KLABU 17 za mchezo wa mpira wa magongo zimethibitisha kushiriki mashindano ya Jamhuri Cup mjini Mombasa wikendi ijayo.

Mashindano hayo yanayofahamika rasmi kama MCHA Daikyo Japan Motors Jamhuri yatashirikisha timu 12 za wanaume na tano za wanawake.Yatafanyika Jumamosi na Jumapili katika uga wa Mombasa Sports Club (MSC). Mashindano hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa Chama cha Hoki Nchini (KHU), Chama cha Hoki Kaunti ya Mombasa (MCHA) na MSC.

Katibu wa MCHA, Feisal Yasin Hussein, asema klabu zilizothibitisha kushiriki katika kitengo cha wanaume ni wenyeji MSC, Daikyo Heroes, Mombasa West, Mvita XI, Kenya Police na Green Sharks.Pia kuna Taskforce, Western Jaguars, Underdogs, Black Tankers, Parkroad na KMXV.

Nazo timu za wanawake zilizokuwa zimetuma hakikisho la kushirki ni pamoja na wenyeji MSC Women, The Swans, Amira Sailors, Blazers, KWXV na Wolverines.Hussein aliambia Taifa Spoti kuwa ratiba ya mechi itatolewa na KHU kuambatana na kanuni za chama.

Kamati andalizi bado inasubiri wanaume wa Parklands, na wanawake wa Chuo Kikuu cha USIU pamoja na Scorpions ya Strathmore kuthibitisha kushiriki kinyang’anyiro hicho. Kwa wachezaji watakaowakilisha timu zao, watahitajika kuwa na hati ya kuthibitisha wamepokea chanjo ya Covid-19.

“Tunaomba maafisa wa klabu za bara pia watumie dawa za kuzuia maradhi ya malaria,” akasema Hussein na kuzikumbusha kuwa zitagharamia usafiri wao.Wakati huo huo, Ligi Kuu ya Hoki (KHU) yatarajiwa kurejea mwezi Februari.Mwenyekiti wa KHU,

Nahashon Randiek, alisema kwanza watakutana na klabu za ligi kuamua tarehe mahususi ya kuanza kwa msimu mpya kwani ule wa 2019/2020 ulikuwa umechezwa michuano miwili au mitatu hivi.. Ligi hiyo ilisitishwa Machi 2020 baada ya virusi vya corona kutua nchini.

Mechi zingerejelewa Aprili mwaka huu lakini zilipigwa breki tena serikali ilipotangaza kuongeza kipindi cha kafyu. “Wachezaji wa timu ya taifa ya wanaume na wanawake wanaendelea na mazoezi kujiandaa kwa Kombe la Afrika mwezi Januari jijini Accra, Ghana.

“Hivyo mechi za Ligi Kuu na Supa zitaanza Februari mwaka ujao,’’ akasema.Aliongeza kwamba klabu zitakuwa na muda mwafaka kujiandaa. Kocha wa wafalme wa zamani Kenya Police, Patrick Mugambi, amepongeza hatua ya ligi kurejea mwaka ujao kwani watapata muda wa kujiandaa, ingawa alisema wao hupiga tizi ili kujiweka fiti.

Police ni kati ya timu 14 ambazo zimethibitisha kushiriki shindano la Jamhuri Cup jijini Mombasa wikendi.Timu hiyo ndio mabingwa watetezi kitengo cha wanaume, nao Scorpions wa Strathmore upande wa kinadada katika kombe hilo.

You can share this post!

Ni kufa au kupona kwa Barca leo UEFA

Ethiopia yatangaza hatua dhidi ya TPLF

T L