Michezo

Klabu anayochezea Malcolm Mamboleo yakamilisha ligi ya raga katika nafasi ya nne

September 12th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Dinamo Bucuresti anayochezea mchezaji wa kimataifa wa raga wa Kenya, Malcolm Mamboleo Onsando, imekamilisha Ligi Kuu ya raga nchini Romania katika nafasi ya nne, Jumamosi.

Mabingwa mara 16 Dinamo wamepoteza mechi ya kuwania medali ya shaba dhidi ya majirani Steaua Bucuresti kwa alama 33-13.

Dinamo, ambayo ililimwa 76-19 dhidi ya Baia Mare katika nusu-fainali hapo Septemba 5, ilienda mapumzikoni dhidi ya Steaua alama 19-3 chini na kushindwa kabisa kujinasua.

Timu ya Dinamo ilitinga nusu-fainali kwa kulaza Chuo Kikuu cha Cluj kwa alama 20-13 hapo Agosti 30.

Mabingwa watetezi Baia Mare waliingia nusu-fainali moja kwa moja kwa kushinda msimu wa kawaida.

Washikilizi wa rekodi ya mataji mengi Steaua Bucuresti pia walijikatia tiketi ya kushiriki nusu-fainali moja kwa moja baada ya kukamilisha msimu wa kawaida katika nafasi ya pili.

Steaua, ambao wanajivunia mataji 24, waduwazwa na Timisoara Saracens 21-20 katika nusu-fainali ya pili mnamo Septemba 6. Fainali ya ligi hii itakutanisha Baia Mare na Timisoara baadaye Septemba 12.

Onsando,25, ambaye amechezea Kenya Simbas tangu Mei 26 mwaka 2018, alijiunga na Dinamo mapema mwaka 2020 akitokea Kenya Harlequin.