Michezo

Klabu anayochezea Mkenya Arnold Origi yafufua matumaini ya kusalia Ligi Kuu Finland

October 24th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HIFK Fotboll anayochezea kipa Mkenya Arnold Origi imefufua matumaini yake ya kukwepa kuangukiwa na shoka kwenye Ligi Kuu ya Finland baada ya kulima Rovaniemi 1-0 Oktoba 22, 2020.

Ushindi huo wa kwanza wa HIFK katika mechi nane ulipatikana kupitia bao la mshambuliaji wa kati wa Gambia, Foday Manneh dakika tatu baada ya kipindi cha pili kuanza katika uwanja wao wa nyumbani wa Bolt Arena jijini Helsinki.

Uliwezesha HIFK kuruka SJK na kutulia katika nafasi ya saba kwa alama 28 kutokana na mechi 21. HIFK sasa iko alama moja ndani ya mduara hatari wa kutemwa kwenye ligi hiyo ya timu 12. Rovaniemi inavuta mkia kwa alama tano baada ya kusakata idadi sawa ya michuano. Origi,36, alikuwa akidakia HIFK mechi ya 11 mfululizo. HIFK pia imeajiri mshambuliaji Mkenya Sydney Lokale, ambaye amekuwa nje kwa miezi kadhaa akipona goti baada ya kufanyiwa upasuaji mwezi Julai.

HJK inaongoza jedwali kwa alama 44 kutokana na mechi 20 ikifuatiwa alama tatu nyuma na KuPS, ambayo imesakata michuano 21. Origi alijiunga na HIFK kutoka Kongsvinger nchini Norway mnamo Machi 9 mwaka 2019 kwa kandarasi itakayokatika Desemba 31, 2020.

Aliitwa na kocha Francis Kimanzi katika kikosi cha timu ya taifa ya Kenya kilichopiga Chipolopolo ya Zambia 2-1 jijini Nairobi mnamo Oktoba 9. Hakusafiri nchini Kenya kwa mechi hiyo kutokana na masharti makali ya usafiri ya Finland wakati huu wa janga la virusi vya corona.

Harambee Stars ilitumia mchuano huo kujiandaa kuvaana na wanavisiwa wa Komoro katika mechi mbili zijazo za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2021 zitakazosakatwa mwezi ujao mnamo Novemba 11 (Nairobi) na Novemba 15 (Moroni).

Naye beki Clarke Oduor, ambaye alishiriki mechi dhidi ya Chipolopolo, alicheza mchuano mzima timu yake ya Barnsley ikitoka 2-2 dhidi ya wenyeji Stoke City kwenye Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uingereza hapo Alhamisi. Stoke ilikamilisha mechi wachezaji 10 baada ya Nathan Michael Collins kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 60.