Michezo

Klabu mpya KPL zazidi kudhalilishwa uwanjani

March 12th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO
KLABU zilizopandishwa kushiriki ligu kuu ya KPL msimu uliopita na ule wa juzi zimeangukia pua kwenye mechi za wikendi iliyopita na kudhihirisha wazi unyonge wao mbele ya mibabe wa ligi hiyo.
Timu hizo aidha ziliangukia sare tasa na kuthibitisha kauli ya wachanganuzi wa soka kwamba zina ubutu mbele ya lango la wapinzani wazoefu au mastraika wao hawana uzoefu wa kufuma magoli.
Klabu ya Nakumatt FC waliomaliza ligi ya daraja la pili msimu uliopita katika nafasi ya pili walinyeshewa mvua ya mabao na wapinzani wao Chemeli.
Wanasupamaketi hao walizidiwa maarifa kwa kucharazwa 4-0 na vijana hao wa Kocha Patrick Odhiambo.
Hali sawia  na hilo iliwakuta klabu ya Kakamega Homeboyz ambayo ilitandikwa 1-0 na mabingwa wa zamani ulinzi stars wanaotiwa makali na kocha Dunstone Nyaudo aliyechukua majukumu ya kunoa timu hiyo mwezi Disemba mwaka 2017.
Wenzao Klabu ya Nzoia FC hawakusazwa baada ya kupigwa 1-0 na mabingwa mara 16 Gormahia uwanjani Kenyatta kaunti ya Machakos. Japo Nzoia FC walipigana kiume na kuonyesha mchezo uliokwenda skuli bahati haikuwa upande wao na bao lake Kevin Omondi lilitosha kuwanyima alama zote tatu.
Matokeo mengine yalishuhudia timu  za Vihiga United,Wazito Fc,Kariobangi Sharks na Zoo Kericho FC zikiambulia sare tasa dhidi ya wapinzani wao.
Kwenye msimamo wa jedwali la ligi  klabu hizo zinamiliki nafasi tano za chini.Ni klabu za Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboyz pekee zinazomiliki nafasi ya nane na kumi mtawalia.
Nzoia FC,Zoo Kericho na Vihiga United zinakalia  nafasi za tatu za mwisho nao Wazito FC na Nakumatt FC zikiwa nambari 14 na 13 mtawalia.