Klabu ya Al-Nassr nchini Saudi Arabia yaweka mezani Sh25.8 bilioni kwa ajili ya maarifa ya Cristiano Ronaldo

Klabu ya Al-Nassr nchini Saudi Arabia yaweka mezani Sh25.8 bilioni kwa ajili ya maarifa ya Cristiano Ronaldo

Na MASHIRIKA

KLABU ya Al-Nassr iliyoko Saudi Arabia imeweka mezani ofa nono ili kujitwalia huduma za nyota Cristiano Ronaldo baada ya fainali za Kombe la Dunia kukamilika nchini Qatar.

Japo vikosi kadhaa vinawania maarifa ya sogora huyo wa zamani wa Manchester United, Juventus na Real Madrid, ni Al-Nassr ambao wametoa ofa kubwa zaidi – ya Sh25.8 bilioni.

Ronaldo, 37, sasa yuko huru kujiunga na kikosi chochote kuanzia Januari 2023 baada ya kukatiza mkataba wake na Man-United mnamo Novemba 2022.

Mbali na kukosoa waajiri wake, alilalamikia pia kuhangaishwa na vinara wakuu wa Man-United huku akisisitiza kuwa hana heshima yoyote kwa kocha Erik ten Hag ambaye sasa anadhibiti mikoba ya mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Old Trafford.

Katika mahojiano yake na TalkTV mnamo Novemba 2022, Ronaldo pia alifichua kwamba aliwahi kutupilia mbali ofa ya kujiunga na kikosi kimoja cha Saudi Arabia kwa Sh45.4 bilioni.

Inaaminika kwamba kwa sasa Ronaldo analenga kumakinikia zaidi kampeni za Ureno kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar na hana nia ya kufanya maamuzi yoyote kuhusiana na mustakabali wake kitaaluma hadi kivumbi hicho kitakapotamatika.

“Tumekuwa tukimezea Ronaldo mate kwa muda mrefu. Tungependa sana kumsajili ila tunaelewa kwamba kwa sasa mawazo yake yote yangali kwa Kombe la Dunia ikizingatiwa kwamba yeye ni tegemeo la Ureno,” akaeleza msemaji wa Al-Nassr.

Ureno wameratibiwa kumenyana na Uswisi katika pambano la hatua ya 16-bora kwenye Kombe la Dunia mnamo Disemba 6, 2022.

Mwanzoni mwa fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, Ronaldo aliweka rekodi ya kuwa mtu wa kwanza kuwahi kufunga bao katika makala matano tofauti ya Kombe la Dunia baada ya kupachika wavuni penalti na kuongoza Ureno kuzamisha Ghana 3-2.

Japo ni mchezaji huru kwa sasa asiye na klabu yoyote, hana idhini ya kusajiliwa na klabu nyingine yoyote hadi Januari 1 kwa mujibu wa kanadarasi yake ya awali na Man-United waliomsajili upya mwanzoni mwa muhula wa 2021-22.

Ronaldo pia anatakiwa kutumikia marufuku ya mechi mbili katika klabu yoyote ikatakayomsajili baada ya kuadhibiwa na Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) kwa kosa la kurusha chini simu kutoka kwa mkono wa shabiki mmoja wa Everton msimu uliopita wa 2021-22.

Ronaldo alifunga mabao 145 kutokana na mechi 346 akivalia jezi za Man-United kabla ya kuyoyomea Real Madrid mnamo 2009 na kurejea ugani Old Trafford baada ya kuagana na Juventus mnamo 2021.

Akiwa Man-United, alikuwa akidumishwa kwa mshahara wa Sh74.5 milioni kwa wiki.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

TSC yasifu walimu kujitolea kisiwani

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Brazil kuvaana na Croatia kwenye...

T L