Klabu ya Masud Juma yaendelea kuzama Ligi Kuu Morocco

Klabu ya Masud Juma yaendelea kuzama Ligi Kuu Morocco

Na GEOFFREY ANENE

DIFAA Hassani Jadidi (DHJ) anayochezea mshambuliaji Masud Juma imechabangwa 2-0 na wenyeji Berkane kwenye Ligi Kuu ya Morocco, Jumatatu.

Mkenya huyo alikuwa kikosi cha DHJ ambacho kilitawala idara nyingi tu kwenye mchuano huo.

Wageni hao walikuwa na umilikaji wa mpira kwa asilimia 51 dhidi ya 49, majaribio ya langoni tisa dhidi ya saba, makombora yaliyokosa lango nane kwa tatu na frikiki 21-10, miongoni mwa takwimu nyingine nzuri. Hata hivyo, walikosa bahati na kuzamishwa kupitia mabao ya mshambuliaji Hamdi Laachir dakika ya tatu na kiungo Alain Traore dakika ya 51.

DHJ sasa haina ushindi dhidi ya Berkane katika michuano minane. Timu hizi zilikuwa zimetoka sare mara nne mfululizo kabla ya Berkane kudumisha rekodi ya kutoshindwa nyumbani na wapinzani hawa hadi mechi 11. Mara ya mwisho DHJ ilipata ushindi ugenini dhidi ya Berkane ni Novemba 2012 ilipolima wenyeji wake 1-0.

Wydad inakamata nafasi ya kwanza kwa alama 26 baada ya kujibwaga ugani mara 12. Raja Casablanca imezoa pointi 25 nayo Hassania Agadir ya nne zikiwa zimeambulia alama 25 na 20 kutokana na mechi 13 kila mmoja.

  • Tags

You can share this post!

Erzurumspor anayochezea Omolo yaendelea na ufufuo Ligi Kuu...

WINNIE ONYANDO: Simu ya mwenzio sumu