Michezo

Klabu yatumia madoli kama 'Samantha' yawe 'mashabiki'

May 18th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KLABU ya FC Seoul nchini Korea Kusini imeomba msamaha kwa kutumia madoli kama ‘Samantha’ kujaza viti ambavyo kwa kawaida, hukaliwa na mashabiki wanaofika uwanjani kuhudhuria mechi.

Shughuli za soka zimeanza kurejelewa katika baadhi ya mataifa kama vile Ujerumani, Korea Kusini na Belarus licha ya janga la corona kutodhibitiwa vilivyo duniani.

Hata hivyo, mchezo huo wa mpira wa mguu unaopendwa sana utakuwa ukipigwa ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki.

Katika soka ya Ujerumani na Belarus kwa mfano, ni watu wasiozidi 322 ndio wamekuwa wakiruhusiwa ugani huku muziki unaochezwa kwenye vyombo ukihanikiza anga za viwanja ambavyo vilikuwa vimezoea mbwembwe na hekaheka za mashabiki waliojitokeza kutilia shime wanasoka.

Kwa mujibu wa mtandao wa rt.com, FC Seoul ilijaza madoli kwenye viti vya uwanja wao wa nyumbani mnamo Mei 17, 2020, kabla ya mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Gwangju FC.

Ilihitaji macho makali ya mashabiki kutambua kwamba madoli hayo yalikuwa ya mapenzi na punde wakajibwaga kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kutaka kujua kiini cha hatua hiyo ya FC Seoul ambayo awali usimamizi ulisisitiza kwamba walikuwa wakitangaza mavazi mbalimbali ambayo madoli hayo yalivalishwa.

Ingawa cha kushangaza ni jinsi mashabiki walivyobaini kwamba madoli hayo hutumiwa katika masuala ya ngono, vinara wa FC Seoul wamekiri makosa na kutumia mtandao wa Instagram kuomba radhi huku wakishikilia kwamba mkandarasi aliyetakiwa kuupamba uwanja wao kwa madoli ya kawaida, alichanganyikiwa.

Shabiki mmoja aliyetambua matumizi halisi ya madoli hayo kabla ya FC Seoul kuomba msamaha alisema: “Nimeshangaa kuona madoli ya ngono katika uwanja. Hayo ni madoli ambayo yaliwahi pia kujaribiwa na kikosi cha Dinamo Brest. Ni kana kwamba ‘mashabiki’ hawa wa FC Seoul ni ‘madoli ya ngono’. Itakuwa aibu kubwa iwapo ni kweli.”

Shabiki mwingine alisema, “Hebu fikiria mchakato mzima wa kujaza madoli ya ngono yenye maumbo ya wanawake kwenye viti vya uwanja mzima na kuyavisha jezi za wanasoka. Je, hilo ni wazo bovu kweli? Ni wazo tamu mno. Hongereni sana @FCSeoul.”