Michezo

Klabu za mabinti zachangamkia udhamini wa Betking

August 24th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU zinazoshiriki kampeni za Ligi Kuu ya Soka la Wanawake la Kenya (KWPL) zinachangamkia udhamini wa kampuni ya kamari ya BetKing na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ambapo kipute hicho kitapokea Sh60 milioni ndani ya miaka mitano.

Kocha wa klabu ya Eldoret Falcons, Joshua Ariko amesema ingawa hawaelewi uhalali wa dili hiyo pia udhamini huo haujaanza kutekelezwa hawana budi kumpongeza rais wa shirikisho hilo, Nick Mwendwa.

Naye katibu wa FKF, Tawi la Nairobi Magharibi, Caleb Malweyi vile vile amepongeza rais wake kwa kupiga hatua hiyo. Alhamisi iliyopita, FKF ilitangaza kuwa imeingia dili na kampuni hiyo kutoa udhamini wa kitita cha Sh1.2 bilioni ndani ya miaka mitano.

SH 12 MILIONI

”Kando na udhamini huo kuelekezwa kwa kipute cha Ligi Kuu Kenya (KPL) ya wanaume kila msimu timu zinazoshiriki ligi kuu (KWPL) zitakuwa zinapokea jumla ya Sh12 milioni maana hatuna mfadhili mwingine,” Mwendwa alisema na kuongeza kwamba endapo watapata ufadhili mwingine pia watagawia klabu ambazo hushiriki mechi za Betka Supa Ligi ya Taifa (BNSL).

Kampuni hiyo itaanza kutoa ufadhili huo kuanzia Septemba mwaka huu baada ya kampeni za muhula ujao kungóa nanga. Hata hivyo bosi wa Kakamega Homeboyz ambayo hushiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kitengo cha wanaume anakosoa Mwendwa kwa kutoshauriana na klabu za kipute hicho kabla ya kusaini mkataba huo.

KUNOA MAKUCHA

Katibu huyo aliliambia Mwanaspoti kuwa mkataba huo utapaisha soka la Kenya maana pia utaweka matumaini ya wadhamini zaidi kwa vipute vya chini ili kunoa makucha ya wapigagozi wanaokuja.

”Kusema kweli viongozi wa matawi ya FKF kote nchini tumefurahishwa na dili hiyo maana itasaidia klabu ambazo hushiriki vipute hivyo. Kenya ina wachezaji wazuri lakini ukosefu wa udhamini huzima mikakati yao michezoni.”

Katika mpango mzima soka la wanawake nchini limeonekana limeanza kuimarika hasa baada ya rais wa FKF kutwaa hatamu ya kuongoza shirikisho hilo miaka minne iliopita.

KIMATAIFA

”Ingawa udhamini huwa hautoshi bila shaka utasaidia pakubwa soka la wanawake nchini na kuwatia washiriki motisha kujituma michezoni. Wachana nyavu wa kike nchini huwa hawamo fomu moja na wanaume hatua ambayo hudidimiza jitihada zao Viwanjani,” Ariko alisema.

Naye kocha wa Ulinzi Starlets, Joseph Wambua Mwanza anasema kwa jumla udhamini huo utaimarisha na kuboresha zaidi viwango vya ushindani miongoni mwa washiriki wa kipute hicho nchini.

”Hakika endapo ligi yetu nitafanikiwa kupata wadhamini Kenya haitakuwa na budi ila itaendelea kutoa wachezaji wengi tu kujiunga na soka la kulipwa katika mataifa ya ughaibuni,” alisema.

Tangu Mwendwa na naibu wake, Doris Petra wachanguliwe kuongoza FKF wasichana kadhaa wanashiriki mchezo huo katika mataifa ya kigeni akiwamo Mbeyu Akida (Besiktas, Uturuki), mnyakaji Annete Kundu na beki Ruth Ingosi wote (Lakatamia, Cyprus). Mwingine akiwa Vivian Corazone Odhiambo ambaye husakatia Atletico Ouriense ya Ureno.