Michezo

Klabu za UEFA zapata hasara ya Sh860 bilioni

June 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

VIKOSI vinavyoshiriki soka ya bara Ulaya vitapoteza kima cha Sh490 bilioni kutokana na janga la virusi vya corona hata iwapo ligi kuu za mataifa mbalimbali na vipute vya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Europa League vitakamilishwa msimu huu.

Hesabu hiyo ya fedha ambazo zitapotezwa kuanzia sasa hadi mwishoni mwa msimu ujao, ilifichuliwa katika mkutano ulioandaliwa na vinara wa soka ya bara Ulaya (Uefa) mnamo Juni 2, 2020.

Inakadiriwa kwamba huenda kiasi hicho cha fedha kikaongezeka hadi kufikia Sh860 bilioni iwapo kampeni za UEFA na Europa League zitafutiliwa mbali muhula huu.

Ligi Kuu ya Ujerumani ilirejelewa wikendi iliyopita ya Mei 16, 2020 na zile za Uhispania (La Liga), Italia (Serie A) na Uingereza (EPL) zinatazamiwa kuanza upya kufikia Juni 20. Kufikia sasa, Ligi Kuu za Uholanzi (Eredivisie) na Ufaransa (Ligue 1) zimetamatishwa na vinara wa soka wa mataifa hayo kwa mashauriano na serikali zao.

Ukubwa wa hasara hiyo ambayo itapata klabu husika za soka barani Ulaya unatarajiwa kuwa kiini cha kufanikishwa kwa mipango ya kukamilisha misimu ya kampeni zote zilizopo na kuendeleza soka ya muhula ujao.

Mtihani mkubwa zaidi hata hivyo ni jinsi ya kuratibu jumla ya michuano 203 ya mikondo miwili ya kufuzu kwa UEFA na Europa League miongoni mwa mataifa 55 wanachama wa Uefa kufikia katikati ya Oktoba 2020.

Licha ya changamoto nyingi za kimpangilio, kiafya, kisiasa na kifedha; vinara wa soka ya bara Ulaya wameshikilia uwezekano wa kusakatwa kwa fainali ya kivumbi cha UEFA katika msimu huu wa 2019-20 mnamo Agosti 29.

Waendeshaji wa kipute hicho wameratibiwa kukutana Mei 20, 2020 ili kujadili mustakabali wa mechi zilizosalia katika kalenda ya muhula huu ambayo imeathiriwa pakubwa na virusi vya homa kali ya corona.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, huenda waandalizi wa UEFA wakaafikiana kuendelezwa kwa kinyang’anyiro hicho baada ya Ligi Kuu zilizosalia barani Ulaya; yaani EPL, Bundesliga, La Liga na Serie A kutamatika rasmi.

“Kubwa zaidi kwa sasa ni kuona jinsi ambavyo kampeni zote za Europa League na UEFA msimu huu zitakavyotamatika kufikia mwisho wa Agosti 2020,” akasema Rais wa mashindano hayo ya bara Ulaya, Aleksander Ceferin.

Iwapo mtazamo wa Ceferin utakumbatiwa na wadau wengine katika kikao kijacho, basi huenda fainali ya UEFA ikaandaliwa jijini Istanbul, Uturuki mnamo Agosti 29, siku tatu baada ya kutandazwa kwa fainali ya Europa League jijini Gdansk, Poland.

Hata hivyo, kufanikiwa kwa mipango hiyo kutamaanisha kwamba mikondo miwili ya michuano ya robo-fainali na nusu-fainali itasakatwa kama mechi za kawaida katikati ya ratiba ya Ligi Kuu za mataifa husika wakati wowote kati ya Julai na Agosti.

Namna nyingine itakuwa ni kuandaliwa kwa michuano ya mkondo mmoja pekee katika hatua za robo-fainali na nusu-fainali baada ya kampeni za Ligi Kuu zote tano za bara Ulaya kutamatishwa rasmi mwishoni mwa Julai.

Nne kati ya klabu nane za robo-fainali za UEFA tayari zinajulikana kufikia sasa huku kivumbi cha haiba kati ya Manchester City na Real Madrid kikisalia na mkondo mmoja zaidi kabla ya atakayesonga mbele kujulikana.

Kizungumkuti kikubwa zaidi kipo katika jinsi ya kuratibu mechi za kivumbi cha Europa League kwa sababu michuano yote minane katika hatua ya 16-bora bado haijachezwa huku mechi mbili za mkondo wa kwanza zinazohusiaha klabu za Uhispania na Italia zikiwa bado hazijapigwa.

Vikosi vya Manchester City na Chelsea kutoka Uingereza ndivyo vingalipo katika kivumbi cha UEFA huku Manchester United, Wolves na Rangers kutoka Scotland zikiwa miongoni mwa timu ambazo bado zinawania ufalme wa Europa League muhula huu.

Katika mechi nyinginezo za mkondo wa pili wa UEFA, Juventus watavaana na Lyon, Barcelona wapimane ubabe na Napoli nao Bayern Munich wagaragazane na Chelsea.