Klabu zote sita za EPL zilizokuwa zimejiunga na European Super League (ESL) zajiondoa kwenye kipute hicho kipya

Klabu zote sita za EPL zilizokuwa zimejiunga na European Super League (ESL) zajiondoa kwenye kipute hicho kipya

Na MASHIRIKA

KLABU sita za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zilizokuwa zimejiunga na pambano jipya la European Super League (ESL) sasa zimejiondoa rasmi kwenye kipute hicho.

Manchester City walikuwa wa kwanza kujitoa rasmi kwenye kivumbi hicho baada ya Chelsea kufichua mpango wa kufanya hivyo kwa kuandaa stakabadhi za kujiondoa kwao.

Klabu nne nyinginezo – Arsenal, Liverpool, Manchester United na Tottenham Hotspur zilifuata mkondo. Tangazo la kuundwa kwa kivumbi kipya cha ESL kikijivunia ushiriki wa vikosi 12 vya kwanza lilitolewa rasmi mnamo Jumapili na kuzua hisia mseto kutoka kwa wadau wa soka duniani wakiwemo mashabiki, vinara wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Man-City ambao kwa sasa wanaongoza jedwali la EPL, wamethibitisha kwamba “wametekeleza hatua zote muhimu katika mchakato wa kujiondoa” kwenye ESL.

Kwa upande wao, Liverpool walisema kwamba kuhusika kwao kwenye kivumbi hicho “kumesitishwa rasmi.”

Man-United walisema walikuwa “wamesikiliza zaidi hisia zilizotolewa na mashabiki wao, Serikali ya Uingereza na washikadau wengine muhimu” kabla ya kufanya maamuzi ya kujiondoa.

Arsenal walitumia barua kuomba radhi kutoka kwa mashabiki wao wakisema “lilikuwa kosa kuingia katika kipute cha ESL” huku wakisisitiza kwamba kujiondoa kwao kulifanyika baada ya kusikiliza “jamii pana ya wapenzi wa soka.”

Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy, kwa upande wake alisema anajutia “mchecheto na usumbufu” uliosababishwa na pendekezo la kubuniwa kwa pambano la ESL.

Mbali na vikosi hivyo sita vikuu vya EPL, klabu nyinginezo zilizohusishwa katika kuundwa kwa kivumbi cha ESL ni Atletico Madrid, Barcelona na Real Madrid za Uhispania pamoja na AC Milan, Inter Milan na Juventus za Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Takriban mashabiki 1,000 wa Chelsea walikongamana nje ya uwanja wa Stamford Bridge kulalamikia hatua ya kikosi chao kujiunga na ESL kabla ya kupigwa kwa mchuano wa EPL kati ya kikosi hicho cha kocha Thomas Tuchel na Brighton waliowalazimishia The Blues sare tasa.

Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Man-United, Ed Woodward, aliyehusika pakubwa katika mjadala wa kuanzishwa kwa ESL ametangaza kwamba atajiuzulu kwenye wadhifa wake mwishoni mwa mwaka huu wa 2021.

Miongoni mwa wachezaji katika klabu sita kuu za EPL waliopinga pia hatua ya kubuniwa kwa kipute cha ESL ni nahodha wa Liverpool, Jordan Henderson na mshambuliaji matata wa Man-City, Raheem Sterling.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Mahangaiko ya wananchi waliobomolewa makao...

Watford wahitaji alama nne pekee kutokana na mechi tatu...