Habari Mseto

Kliniki ya Murugu motoni kwa kuuza sumu

June 18th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYAKAZI saba wa kiliniki ya mitishamba ya Murugu walishtakiwa Jumanne kwa kupatikana na dawa sisizosajiliwa na kuuza sumu kinyume cha sheria.

Saba hao Catherine Nduta Warui, Diana Wanjiku Wahu, Saida Mariam Zakaria, Henry Mukhwana Mukunga, Samuel Kamau Ng’ang’a na Francis Maina Ndumia walishtakiwa katika mahakama ya Milimani.

Walikanusha mashtaka matatu walipofikishwa mbele ya hakimu mkazi Bi Muthoni Nzibe.

Mashtaka dhidi yao yalikuwa ni kutengeneza dawa za miti shamba bila kibali kutoka Bodi ya Kitaifa kuhusu Dawa na Sumu  kinyume na sheria nambari 244, sehemu ya 35A na 51 ya sheria za sumu na madawa.

Washtakiwa walidaiwa mnamo Juni 17, 2019 katika Kliniki cha Murugu Natural & Nutritional kilichoko barabara ya Moi jijini Nairobi, walihifadhi madawa mbalimbali bila leseni.

Shtaka la pili lilisema kuwa washukiwa hao walipatikana wakiuza madawa katika Kliniki cha Murugu barabara ya Moi, Kaunti ya Nairobi ambayo hayakuwa yameandikishwa na Bodi ya Madawa ya Serikali.

Washtakiwa hao walikabiliwa na shtaka la tatu kwamba waliuza dawa katika mikebe isiyo na majina ya dawa.

Washtakiwa hao walikana mashtaka dhidi yao na kuomba waachiliwe kwa dhamana.

“Sipingi washtakiwa wakiachiliwa kwa dhamana ila naomba mahakama izingatie washtakiwa walikuwa wakiuza dawa sisizotambuliwa na Serikali ambazo ni hatari kwa afya ya umma,”wakili wa Serikali anayeongoza mashtaka alimweleza Bi Nzibe.

Akitoa uamuzi, Bi Nzibe alisema, “Dhamana ni haki kwa kila mshukiwa kwa mujibu wa Kifungu nambari 49 cha Katiba.”

Bi Nzibe alisema kesi inayowakabili washtakiwa ni mbaya ikitiliwa maanani inahusu afya ya wananchi.

Aliamuru kila mmoja wa washukiwa hao saba wawasilishe dhamana ya Sh500,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho ama walipe dhamana ya pesa tasilimu Sh200,000 kila mmoja kabla ya kuachiliwa kutoka gerezani.

Mahakama ilitenga Julai 16 siku ya kusikizwa kwa kesi dhidi yao.