Michezo

Klopp aambia Liverpool, tulieni taji lingali mbali

January 21st, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema kuwa japo anafurahia msisimko wa mashabiki wa klabu hiyo wanaozidi kuamini kuwa timu yao itashinda Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu, anasisitiza kuwa lengo lake linabakia kwa kila mechi jinsi ijavyo.

Hii ni baada ya Liverpool kuwamenya mahasimu wao wa tangu jadi Manchester United kwa kuwapiga mabao 2-0 ugani Anfield mnamo Jumapili.

Baada ya kipenda cha mwisho, mashabiki wa Liverpool waliimba, “tutashinda ligi, tutashinda ligi” huku kikosi hicho maarufu kama The Reds kikikaribia kutwaa taji lake la kwanza la ligi hiyo katika muda wa miaka 30.

“Wanaweza kuimba hivyo,” akasema Klopp.

“Siko hapa kuwaamulia wanachotaka kuimba. Iwapo mashabiki wetu hawangekuwa na msisimko huo mkuu, basi hilo ndilo kwa kweli lingekuwa tatizo. Bila shaka wanaruhusiwa kuota ndoto na kuimba wanachopenda, almradi wanatekeleza jukumu lao huku sisi tukicheza, hamna tatizo. Lakini hatuwezi kuanza kusherehekea nao kwa sasa.”

Ushindi huo umewawezesha vijana hao wa Klopp kuogoza msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 16, hata wakiwa na mechi moja kibindoni.

Liverpool walicheza vizuri, hasa baada ya kupata bao la kwanza kupitia kwa beki Virgil van Dijk aliyefunga kwa kichwa dakika ya 14 kutokana na kona, lakini wakalemewa zaidi mechi hiyo ikielekea kumalizika.

Mohamed Salah aliongeza bao la pili katika muda wa majeruhi baada ya kuandaliwa mpira na kipa wao Alisson.

Washindi hao wangemaliza mechi hiyo kwa mabao matatu kama mtambo wa VAR ungekubali bao la Roberto Firmino. Bao hilo lilikataliwa baada ya VAR kuonyesha beki Van Dijk akimchezea rafu kipa David de Gea.

Kadhalika, Salah alikosa kufunga bao la wazi kutoka yadi sita pekee baada ya kombora lake kugonga mwamba wa goli na kutoka nje.

Kwa upande mwingine, United ambao watacheza mechi kadhaa bila huduma ya Marcus Rashford aliyeumia katika mechi ya awali, walikuwa na nafasi kadhaa za kufunga mabao lakini hawakufanya hivyo.

Andreas Pereira na Anthony Martial watajilaumu kwa kupoteza nafasi kadhaa wakiwa karibu na lango.

United chini ya Ole Gunnar Solskjaer walicheza kwa bidii katika kipindi cha pili lakini hawakufanikiwa kufunga.

Manchester City wanaendelea kushikilia nafasi ya pili kwa pointi 48, alama 16 nyuma ya Liverpool, lakini tatu mbele ya Leicester City (45), huku Chelsea wakikamata nafasi ya nne (39).

United wanafunga tano bora kwa pointi 34, wakipitwa kwa pointi 30 na vinara Liverpool.