Klopp afutilia mbali uwezekano wa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Ujerumani

Klopp afutilia mbali uwezekano wa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Ujerumani

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool amefutilia mbali uwezekano wa kuwa mrithi wa mkufunzi Joachim Loew atakayeagana rasmi na timu ya taifa ya Ujerumani mwishoni mwa fainali za Euro 2021.

Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) lilitangaza Jumanne kwamba Loew atajiuzulu baada ya kukamilika kwa fainali za Euro zilizoahirishwa kutoka mwaka wa 2020 kwa sababu ya janga la corona.

“Sitakuwa miongoni mwa watakaowania fursa ya kuwa kocha mpya wa Ujerumani. Nadhani kazi hiyo itamwendea mtu mwingine na ninaamini DFB itampokeza mikoba mkufunzi atakayekuwa suluhu kwa matatizo ya kikosi hicho kwa sasa,” akasema Klopp ambaye anahusishwa pakubwa na mikoba ya Bayern Munich na Real Madrid iwapo ataondoka Liverpool.

Klopp, 53, aliteuliwa kuwa mkufunzi wa Liverpool mnamo Oktoba 2015 na akaongoza kikosi hicho kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019 kabla ya kutawazwa wafalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2019-20.

Taji hilo la EPL lilikuwa la kwanza kwa Liverpool kunyanyua baada ya ukame wa miaka 30. Hata hivyo, mabingwa hao watetezi wa EPL wanaandamwa na masaibu tele muhula huu.

Wanashikilia nafasi ya nane jedwalini kwa alama 43 baada ya kupoteza jumla ya michuano sita iliyopita kwa mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani wa Anfield. Matokeo hayo yanadidimiza matumaini yao ya kumaliza kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na hatimaye kufuzu kwa mapambano ya UEFA muhula ujao.

“Haiwezekani kabisa niwe kocha wa Ujerumani. Ningali na miaka mitatu kwenye mkataba wangu wa sasa na Liverpool. Ni rahisi namna hiyo. Unatia saini kandarasi na unasalia kuwa mwaminifu kwa mkataba huo. Hivyo ndivyo nilivyowahi kufanya awali katika vikosi vya Mainz na Borussia Dortmund,” akaongeza mkufunzi huyo raia wa Ujerumani.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kuvaana na RB Leipzig ya Ujerumani katika marudiano ya hatua ya 16-bora ya UEFA. Mechi hiyo itachezewa jijini Budapest, Hungary mnamo Machi 10, 2021 na Liverpool watajitosa ugani Puskas Arena wakijivunia ushindi wa 2-0 kutokana na mchuano wa mkondo wa kwanza.

Loew, 61, alipokezwa mikoba ya Ujerumani mnamo 2006 baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa Jurgen Klinsmann. Mkataba wake wa sasa na miamba hao wa soka duniani ulitarajiwa utamatike rasmi mwishoni mwa 2022, yaani baada ya fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa nchini Qatar.

Baada ya kuongoza Ujerumani kutwaa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil, Loew alisaidia kikosi hicho kutinga nusu-fainali za Euro 2016 ambapo walibanduliwa na wenyeji Ufaransa.

Alijikuta katika presha kubwa zaidi mnamo 2018 baada ya Ujerumani kuondolewa mapema katika hatua ya makundi kwenye fainali hizo zilizofanyika nchini Urusi.

Ujerumani kwa sasa wako katika Kundi F kwenye fainali za Euro 2021 ambapo wamepangwa pamoja na Hungary, Ufaransa ambao ni mabingwa wa dunia na Ureno ambao ni mabingwa watetezi wa taji la Euro.

Fainali za Euro 2021 zimepangiwa kuandaliwa kati ya Juni 11 na Julai 11 na Ujerumani wataanza kampeni zao dhidi ya Ufaransa mnamo Juni 15 uwanjani Allianz Arena jijini Munich.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Uwanja maarufu wa Maracana nchini Brazil sasa kuitwa Rei...

Manchester City roho juu ikiwaalika Southampton leo...