Michezo

Klopp aivulia Napoli kofia baada ya kumlisha sakafu

September 19th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

NAPLES, ITALLIA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool ameijumuisha Napoli katika orodha ya timu zilizo na uwezo mkubwa wa kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa barani Ulaya, msimu huu.

Licha ya kuanza na mastaa tisa waliokuwa katika kikosi kilichoshinda Tottenham Hotspur na kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya, Liverpool walijipata wakilala 2-0 mbele ya vigogo hao ugenini.

Adrian alijaza nafasi ya kipa Alisson anayeuguza jeraha huku James Milner akianza badala ya Georginio Wilnaldum.

Hata hivyo, wadadisi wamesema kuwa kichapo hicho ni funzo kwa vijana hao wa kocha Klopp baada ya kikosi chake kuendeleza matokeo ya ushindi kwa muda mrefu tangu wanyakue taji la Klabu Bingwa pamoja na ubingwa wa European Super Cup.

Liverpool walicheza vibaya kwenye mechi hiyo ya Kundi E iliyochezewa San Paolo Stadium. Msimu uliopita walifuzu kwa hatua ya 16 Bora kichupuchupu baada ya kupoteza mechi zao zote tatu za ugenini baada ya kukutana na Paris-St Germain pamoja na Napoli katika kundi moja. Lakini mbali na Napoli, timu nyingine za Kundi E ni limbukeni Genk na Salzburg.

Napoli chini ya kocha Carlo Ancelotti walijipatia bao la kwanza kupitia kwa Dries Mertens kutokana na mkwaju wa penalti baada ya Andy Robertson kumchezea ngware Jose Callejon.

Napoli waliongeza bao la pili kupitia kwa Fernando Lllorente mechi ikielekea kumalizika kutokana na makosa ya Virgil van Dijk.

“Napoli walitushinda kwa sababu walikuwa na mpango mzuri wa kupata ushindi, mbali na kujivunia wachezaji wa ujuzi wa mechi kubwa. Ili kutwaa taji la Klabu Bingwa, timu inahitaji kujipanga vyema. Napoli walianza vizuri na wakamaliza vizuri pia. Lazima tukubali walikuwa bora kutuliko.”

“Tumeshindwa, lakini subirini baada ya mechi zijazo mtatuona tukiwa juu. Tutaendelea kujitahidi mazoezini na kurekebisha makosa yaliyotokea,” alisema Klopp.

Kalidou Koulibaly

Maoni ya kocha huyo yaliungwa mkono na mlinzi Kalidou Koulibaly, raia wa Senegal aliyeongoza safu ya ulinzi kwenye mechi hiyo iliyovutia mashabiki wengi.

Koulibaly aliongoza ngome ambayo iliwazima kabisa Roberto Firmino, Mohamed Salah na Sadio Mane.

Koulibaly alisema kikosi chao kitaendelea kucheza kwa bidii huku kikilenga kutwaa ubingwa na mataji mengine msimu huu wa 2019-20.

“Nilirejea mazoezini kama nimechelewa baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) lakini tayari nimeanza kuelewana na wachezaji wapya,” alisema.

“Nitajitolea kwa asilimia 110, kuanzia mechi ya ligi Jumapili dhidi ya Lecce, ugenini,” alisena nyota huyo aliye na umri wa miaka 28.