Michezo

Klopp asema kikosi cha Liverpool kingali imara

July 18th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Liverpool Jurgen Klopp amesema kwamba anafurahia jinsi kikosi chake kilivyo na hatakimbilia kuwasajili wachezaji wenye majina makubwa kwa sababu timu nyingine mahiri zinazoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zinafanya hivyo.

Liverpool FC maarufu kama The Reds wamesajili mchezaji mmoja pekee ambaye ni kinda wa Uholanzi Sepp Van Den Berg mwenye umri wa miaka 17 na Klopp anasema kuna uwezekano finyu kuwa atawaongeza wachezaji wengine kwenye kikosi chake.

“Sisi tumepoa na tunafuatilia namna matukio yanavyoendelea kuchipuka katika fani ya soka. Msimu huu wa uhamisho hautakuwa kubwa kwa Liverpool kwa sababu tumewekeza sana kwa timu hii katika kipindi cha misimu miwili iliyopita. Kwa kweli hatuwezi kutumia pesa nyingi kila mwaka, lazima mambo yawe tofauti,” akasema Klopp.

Akaongeza: “Watu wanazungumza kana kwamba tunaweza kutumia Sh38.6 bilioni au Sh25.7 bilioni kila msimu kwa usajili wa wachezaji kila dirisha la uhamisho wa wachezaji linapofunguliwa. Kwa sasa kuna tu klabu mbili ambazo zinaweza kutumia kiasi hicho cha pesa; nazo ni Barcelona na Real Madrid pekee,

Alisema upo uwezekano kufanya tathmini.

“Tutatathmni iwapo kuna safu ambayo kidogo imekosa kuimarishwa vizuri ili tuongezee mchezaji mmoja. Tuko imara kila idara na wachezaji wetu wapo sawa kiakili. Kwa ufupi, tupo tayari kwa msimu mpya wa 2019/20,” akaongeza Klopp.