Michezo

Klopp atawazwa kocha bora wa mwaka

July 28th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

JURGEN Klopp wa Liverpool ametawazwa Kocha Bora wa Mwaka katika tuzo za Chama cha Wakufunzi wa Soka ya Uingereza (LMA).

Kutuzwa kwa Klopp kulichangiwa na mafanikio yake ya kuongoza Liverpool kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza msimu huu wa 2019-20 baada ya miaka 30 ya kusubiri.

Emma Hayes wa Chelsea alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake baada ya kuwaongoza vipusa wake kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya FA Women’s Super msimu huu.

Mkufunzi Marcelo Bielsa wa Leeds United alitwaa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka katika Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) baada ya kuongoza kikosi chake kurejea katika soka ya EPL baada ya kuwa nje kwa miaka 16.

“Kwa kweli Klopp alistahiki kutuzwa kwa ukubwa wa mchango wake kambini mwa Liverpool msimu huu. Matokeo ya kikosi chake yalikuwa ya kuridhisha na ameambukiza wanasoka wake wote sifa ya kupigana na kiu ya kutaka kuibuka ushindi katika kila pambano,” akasema kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson wakati wa kutuzwa kwa Klopp.

“Klopp, nakusamehe sasa kwa kunipigia simu usiku wa saa tisa unusu kuniarifu kwamba kikosi chako cha Liverpool kimenyanyua ufalme wa EPL. Asante na hongera sana!” akachekesha Ferguson.

Chini ya Klopp, Liverpool walijizolea jumla ya alama 99 katika EPL msimu huu na wakajivunia pengo la alama 18 kati yao na nambari mbili Manchester City.

“Ni fahari tele kutawazwa Kocha Bora na kupokezwa kombe hili ambalo limepewa jina la Sir Alex Ferguson ambaye ni miongoni mwa wakufunzi ninaowastahi sana katika ulingo wa soka,” akasema Klopp ambaye aliandamana kwa hafla hiyo na makocha wasaidizi wa Liverpool; Pep Lijnders, Peter Krawietz, John Achterberg, Vitor Matos, na Jack Robinson.

Bill Shankly, Bob Paisley, Joe Fagan, Sir Kenny Dalglish na Brendan Rodgers ndio wakufunzi wengine wa hivi karibuni kutwaa taji la Kocha Bora wa LMA.

Gemma Davies wa Aston Villa alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka miongoni mwa vikosi vya Ligi za Championship kwa upande wa wanawake.

Mark Robins wa Coventry aliibuka mshindi wa Kocha Bora wa Mwaka katika Ligi ya Daraja la Pili (League One) naye David Artell wa Crewe Alexandra akaibuka Kocha Bora wa Mwaka katika Ligi ya Daraja la Tatu (League Two).