Michezo

Klopp atetea kutoka sare kwa Liverpool dhidi ya Manchester United

October 22nd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool amekiri kwamba sare iliyosajiliwa na kikosi chake dhidi ya Manchester United katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wikendi iliyopita uwanjani Old Trafford ni matokeo waliyoyatarajia na ni ishara ya ukubwa wa kiu yao katika kutawazwa wafalme wa kipute hicho msimu huu.

Kulingana naye, ufanisi huo unatarajiwa kuwapa vijana wake hamasa zaidi ya kuendeleza rekodi ya kusajili matokeo ya kuridhisha katika kampeni zijazo za mapambano mbalimbali.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kwa kipute cha UEFA kitakachowakutanisha na Genk ya Ubelgiji hapo kesho kabla ya kuwaalika Tottenham Hotspur kwa kibarua kingine kigumu cha EPL.

Kwa upande wao, Man-United watakuwa wageni wa Partizan Belgrade ya Serbia katika mchuano wa Europa League mnamo Alhamisi kabla ya kuwaendea Norwich City ligini mwishoni mwa wiki hii.

Liverpool wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 25 huku pengo la pointi 15 likitamalaki kati yao na Man-United wanaoshikilia nafasi ya 13 kwa alama 10 sawa na Everton.

Licha ya kupoteza alama kwa mara ya kwanza katika kivumbi cha EPL msimu huu, Klopp ameonya kwamba kikosi chake hakina “ulazima wa kutandaza gozi la kufurahisha kila mtu kila wakati kitakaposhuka ugani”.

Klopp ambaye pia amewahi kuwanoa Borussia Dortmund nchini Ujerumani, alitoa kauli hiyo kurejelea matamshi ya mkufunzi Ole Gunnar Solskjaer wa Man-United aliyelalamikia rafu ya Liverpool dhidi ya vijana wake katika kipindi cha pili cha mchezo.

Nyota Marcus Rashford aliwaweka Man-United kifua mbele kunako dakika ya 36 kabla ya Adam Lallana kuwasawazishia Liverpool dakika tano kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchuano kupulizwa.

Mechi tisa bila kupoteza

Mchuano huo ulikuwa wa tisa kwa Liverpool kutandaza hadi kufikia sasa msimu huu bila ya kupoteza.

“Vijana waliwajibika vilivyo dhidi ya Man-United katika kipindi cha pili. Walionyesha azma ya kusajili matokeo bora, wakajituma ipasavyo na kutawaliwa na kiu ya kupata ushindi. Juhudi zao ziliwalipa baada ya mabadiliko muhimu katika safu ya kati na mbele,” akasema kwa kusisitiza kwamba sifa za Liverpool kwa sasa zinawaweka katika uwezo mkubwa wa kutawala soka ya Uingereza.

Licha ya Man-United kuwalemea wageni wao katika kipindi cha kwanza, Liverpool ndio waliotamalaki mchezo na kutawala wageni wao katika takriban kila idara.

Man-United waliingia katika mchuano wakiwa na ulazima wa kusajili ushindi ili kujipunguzia presha na kumtoa Solskjaer katika hatari ya kutimuliwa baada ya kikosi chake kusajili msururu wa matokeo duni.