Michezo

Klopp awataka mashabiki wa Liverpool kuvuta subira

June 29th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Jurgen Klopp amewataka mashabiki wa Liverpool kusubiri zaidi hadi “wakati mwafaka” utakapowadia ili washerehekee pamoja ubingwa wao wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kipindi cha miaka 30.

Maelfu ya mashabiki wamekuwa wakikongamana jijini Liverpool, Uingereza tangu Ijumaa licha ya marufuku yanayoharamisha mikusanyiko ya hadhara kutokana na hofu ya kuenea zaidi kwa virusi vya homa kali ya corona.

Zimamoto walilazimika kuzima moto uliowashwa na sehemu ya mashabiki wao nje ya jengo la Liver Building uliopo karibu na uwanja wa Anfield huku maafisa wa usalama wakikabiliana nao katika tukio ambalo kwa sasa limeshuhudia watu 34 wakijeruhiwa huku watatu wakiumia vibaya zaidi.

Klopp amesema “hajapendezwa kabisa” na matukio aliyoyashuhudia pia katika eneo la Pier Head viungani mwa jiji la Liverpool.

Katika barua yake kwa mashabiki wa Liverpool, Klopp ambaye ni mzawa wa Ujerumani alisema: “Mimi pia ni binadamu. Mapenzi yenu kwa klabu hii ni sawa na yangu. Hata hivyo, kwa sasa jambo bora na muhimu zaidi la kufanya ni kuelewa kwamba hatuna majukwaa mwafaka kwa mikusanyiko ya umma.”

“Tuna jukumu la kuhakikisha kwamba tunawalinda wanajamii ambao wapo katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa. Itakuwa busara kubwa iwapo tutawaheshimu maafisa wa afya ambao tunazidi kuwatambua kwa ukubwa wa mchango wao, maafisa wa polisi na vnara wa mamlaka ya jiji la Liverpool ambao wamejitolea kuhakikisha kwamba sisi kama klabu hatukiuki masharti yaliyopo ya kudhibiti msambao wa corona.”

“Tafadhalini – sherehekeeni – lakini mfanye hivyo kwa njia salama na katika sehemu zisizo za umma, ambapo hamtahatarisha maisha ya wanajamii wengine hasa wakati huu wa janga la corona.”

Liverpool ambao walitawazwa mabingwa wa EPL kwa mara ya mwisho mnamo 1990, wamesuta mienendo ya baadhi ya mashabiki waliojumuika nje ya uwanja wa Anfield huku Meya wa jiji la Liverpool, Joe Anderson, akisema matukio ambayo yamekuwa yakishuhudiwa tangu Ijumaa “yanapaka tope jina la klabu na kushusha hadhi ya jiji la Liverpool.”

Makundi mengine ya mashabiki yalionekana nje ya uwanja wa Anfield usiku wa Alhamisi ya Juni 25, 2020 baada ya Chelsea kuwazamisha mabingwa watetezi Manchester City 2-1 katika ushindi uliowapokeza Liverpool ubingwa wa EPL.

“Iwapo mambo yangalikuwa sawa, nisingependa chochote kingine ila kusherehekea na kuandaa gwaride kubwa zaidi kuliko lile tulilolishuhudia baada ya kunyanyua ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mwaka uliopita, ili tujivunie sote kipindi hiki spesheli. Lakini hali hairuhusu kabisa.”

“Tumefanya mengi sana katika vita vya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 na juhudi hizi haziwezi kupotea hivyo. Wakati mwafaka utakapowadia, sote tutasherehekea pamoja, ila kwa sasa tafadhalini salieni nyumbani kadri ya uwezo wenu.”

Klopp pia alikuwa mwingi wa sifa kwa mashabiki ambao upekee wa mchango wao katika kutilia shime kikosi chao kila kiliposhuka dimbani nyumbani na ugenini, ulichangia pakubwa mafanikio yao chini ya Klopp.

“Napenda sana hamasa yenu, nyimbo zenu na azma yenu ya kukataa kushindwa. Kujitolea kwenu, kuelewa kwenu na imani yenu kwa kila jambo tunalolifanya ndizo siri ya ufanisi wetu. Mambo hayo makubwa mnayoyafanya yamekuwa kiini cha motisha yetu katika kila pambano. Mchango wenu katika kushabikia kikosi ndiyo ‘petroli katika tangi’ ya kila mchezaji,” akasema Klopp katika barua yake.