Habari Mseto

KMPDU yasisitiza kubuniwe tume ya kuajiri wahudumu wa afya na kuangazia maslahi yao

May 18th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MUUNGANO wa Madaktari, Watalaamu wa Dawa na Madaktari wa Meno (KMPDU) Jumatatu umesema maslahi na masaibu yanayofika wahudumu wa afya yataangaziwa ikiwa tume ya kuajiri na kuangazia utendakazi wa wahudumu hao itabuniwa.

“Maslahi ya madaktari na wahudumu wote wa afya nchini yataangaziwa tume ikibuniwa,” akasema kaimu katibu mkuu wa muungano huo Dkt Chibanzi Mwachonda katika kikao na wanahabari jijini Nairobi.

Kwa kubuni tume ya wahudumu wa afya, Dkt Mwachonda alisema changamoto zinazowafika zitakuwa zikiangaziwa ili kuepuka migomo ya mara kwa mara.

“Kwa kufanya hivyo, maslahi ya wahudumu wote wa afya yataweza kuangziwa,” akasema.

KMPDU pia imesema Kenya inahitaji wahudumu 2, 590 zaidi wa afya ili kujaza gapu iliyojiri kufuatia mkurupuko wa janga la Covid-19.

Hii ni kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi ya ugonjwa huu pamoja na wanaofariki.

Muungano huo umesema endapo shughuli ya kuajiri wahudumu zaidi haitatekelezwa haraka iwezekanavyo, vituo vya afya vitalemewa na kazi, Dkt Mwachonda akisema wahudumu walioko tayari wanapitia nyakati ngumu.

“Kwa muda wa siku chache zijazo, visa vya Covid-19 Kenya vitavuka 1,000. Awali, tuliweka wazi idadi hiyo ikitimu tutahitaji madaktari 2,590 zaidi. Serikali iharakishe shughuli ya kuwaajiri,” akaeleza katibu huyo.

Dkt Mwachonda alisema shughuli ya kuajiri wahudumu zaidi imekwama, licha ya tangazo la nafasi hizo kuchapishwa.

Kauli ya KMPDU imejiri siku moja baada ya mgomo wa kitaifa wa wahudumu wa afya kote nchini, uliotarajiwa kuanza leo, Jumatatu, kuahirishwa kwa muda wa siku 21.

Mgomo wasitishwa

Viongozi wa miungano mbalimbali kutetea haki za wahudumu wa afya, ukiwemo ule wa wauguzi (KNUN) na Chama cha Maafisa wa Kliniki (KUCO), ilisema imesitisha mgomo kwa muda baada ya kufanya mashauriano na Wizara ya Afya.

“Tumekubaliana kuwa na mpango wa jinsi tutafanya kazi. Viongozi wa miungano wameafikiana na serikali kufikia mwishoni mwa wiki hii wahudumu wote walio chini ya serikali ya kitaifa watapandishwa ngazi,” akasema Seth Panyako, katibu mkuu KNUN.

Bw Panyako alisema kila mhudumu atapandishwa cheo licha ya anakofanyia kazi.

Miungano hiyo hata hivyo imeonya kuwa endapo matakwa ya wahudumu wa afya hayataafikiwa, hawatakuwa na budi ila kufufua mgomo.

“Serikali hujitokeza kujadiliana nasi tunapotoa ilani ya mgomo. Kwa kuwa hatuwezi kuzungumza mgomo uking’oa nanga, tumewapa siku 21, waafikie matakwa yetu,” akasema George Gibore, katibu mkuu KUCO.

Miungano hiyo inataka wahudumu wa afya kufadhiliwa vifaa vya kutosha wanapohudumia wagonjwa wa Covid-19.

Mbali na madaraka na vifaa vya kazi, wahudumu wa afya pia wanataka nyongeza ya marupurupu hasa kutokana na magumu wanayopitia kukabiliana na virusi vya corona.