Habari Mseto

KNBS: Tofauti ya bidhaa zinaouzwa nje na zinazoagizwa imepungua

November 15th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Tofauti ya thamani ya bidhaa zilizouzwa nje na zilizoagizwa inazidi kupungua baada ya kiwango cha bidhaa zilizoagizwa nchini katika muda wa miezi tisa, hadi Septemba kuongezeka hadi Sh860.87 milioni.

Katika kipindi hicho mwaka wa 2017, thamani ya bidhaa zilizoagizwa nchini ilikuwa Sh852.34 kulingana na takwimu kutoka kwa Shirika la Takwimu nchini (KNBS).

Kwa jumla, kiwango cha bidhaa zilizoagizwa nchini kiliongezeka kwa asilimia 2.64 hadi Sh1.33 trilioni, chini ya kiwango cha bidhaa zilizouzwa nje ambacho kilikuwa ni asilimia 5.78, hadi asilimia Sh470.57 bilioni, takwimu za KNBS za hivi punde zinaonyesha.

Kiwango cha chakula kilichoagizwa nchini kilipungua hadi Sh141 bilioni kutoka Sh184 bilioni kutokana na hali nzuri ya hewa iliyowezesha wananchi kuvuna mazao mengi.

Pia, uagizaji wa mashine ulipungua hadi Sh211.11 bilioni ikilinganishwa na Sh245.9 bilioni mwaka uliotangulia. Uagizaji wa magari ulikuwa ni Sh148.96 bilioni ikilinganishwa na Sh145.7 bilioni awali.

Hata hivyo, uagizaji wa mafuta uliongezeka kwa asilimia 27.6 hadi Sh254.22 bilioni ilhali uagizaji wa bidhaa za viwanda uliongezeka kwa asilimia 11 hadi Sh466.51 bilioni.