Habari Mseto

KNEC: Tulinasa maafisa waliojihusisha kwenye udanganyifu wa KCSE

January 8th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

WASIMAMIZI wa vituo kadhaa vya kufanyia mitihani walikamatwa kwa kujihusisha na vitendo vya udanganyifu wakati wa Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nnne (KCSE) mwaka uliopita, 2023.

Kwenye hafla ya kutoa matokeo hayo Jumatatu, Januari 8, 2024 katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi, mjini Eldoret, Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), lilisema baadhi ya maafisa hao walipatikana wakisaidia wanafunzi kushiriki katika udanganyifu kwenye mtihano huo.

Ni hali ambayo imemfanya mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Elimu, Julius Melly, kushinikiza baraza hilo kufanya ukaguzi wa matokeo hayo baada ya kutolewa kwake.

“Tumekuwa tukipata malalamishi ya baadhi ya wazazi kuhusu matokeo yanayotolewa kwa wanao. Ili kuepuka haya, ninairai KNEC kuyafanyia ukaguzi matokeo hayo, ili kuepuka malalamishi kama tuliyoshuhudia wakati wa Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka uliopita,” akasema Bw Melly, ambaye pia ndiye mbunge wa Tinderet.