Michezo

KNH yatoka nyuma kuiadhibu Commercial 3-2

June 10th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ilitoka chini 0-1 na kufaulu kubeba ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Commercial FC kwenye mechi ya Kundi A Ligi ya Taifa Daraja ya Pili iliyopigiwa uwanjani KNH, Nairobi.

KNH ya kocha, George Makambi ilipata ushindani mkali mbele ya wageni wao huku pande zote zikiwinda pointi tatu muhimu. Nayo Uweza FC ambayo hutiwa na kocha, Charles ‘Stam’ Kaindi iliteleza na kuyeyusha alama tatu muhimu ilipodungwa bao 1-0 na Kenafric FC.

Katika matokeo hayo, matumaini ya Balaji EPZ kurukia uongozi wa kipute hicho yaligonga mwamba ilipoagana sare tasa na Kahawa United kwenye patashika iliyochezewa uwanjani Kahawa Baracks, Nairobi.

Amos Kariuki aliiweka Commercial FC kifua mbele dakika ya 35 kabla ya Isiaka Alenje kusawazishia KNH dakika kumi baadaye. Mechi iliendelea kunoga huku Commercial ikipata bao la pili kupitia Silas Rossy.

Kwa mara nyingine, KNH ilisawazisha kupitia Isiaka Alenje alipotikisa wavu kwa mara pili. Dakika tatu kabla ya kipenga cha mwisho, kizaazaa kilizuka katika ngome ya Commercial FC ambapo Brian Otieno aliitingia KNH bao la ushindi.

”Nashukuru vijana wangu maana hatimaye walifanya kazi nzuri licha ya kuonekana kulemewa katika kipindi cha kwanza,” alisema kocha wa KNH na kuongeza kuwa anahitaji ushindi wa mechi tatu hivi ili kujiongezea matumaini ya kuwapiku wapinzani wake na kurukia uongozi wa kipute hicho.

Matokeo hayo yalifanya KNH kupanda hatua kadhaa mbele na kutua tatu bora kwa alama 33. Uweza FC ingali kifua mbele kwa alama 38, moja mbele ya Balaji EPZ.

Kwenye mfululizo wa mechi hizo, Mwiki United ilinyukwa mabao 3-1 na Thika Allstars nayo Magana Flowers iliona giza ilipobugizwa mabao 5-1 na Limuru Olympics.