Habari Mseto

Knut na Kuppet zalaumiana kuhusu anayewajali walimu

September 17th, 2018 2 min read

Na PIUS MAUNDU

KATIBU Mkuu Msaidizi wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Bw Collins Oyuu amekashifu Chama cha Walimu wa Sekondari (KUPPET), kwa walivyowafanya walimu wafutilie mbali mgomo uliopangiwa kufanyika muhula wa tatu ukianza.

Bw Oyuu alidai KUPPET ilikuwa ni kikwazo katika juhudi za kutetea maslahi ya walimu kupitia kwa mgomo ambao ungelemaza masomo muhula huu.

Kulingana naye, KNUT ilikutana na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) wakakubaliana kuwe na mkutano wa kujadili masuala tata yanayokumba walimu, ilhali KUPPET ilipokutana na TSC, ilitoka mkutanoni ikiwa na maelewano tayari.

Bw Oyuu alipuuzilia mbali maelewano kati ya KUPPET na TSC na kusema KUPPET haina nguvu za kutosha, huku akiongeza kuwa makubaliano hayo hayatafua dafu.

“Mliona tukishauriana na TSC kisha tukasema ni lazima tukae tuzungumze zaidi. KUPPET ilifanya nini? Siku hiyo hiyo walikaa na TSC wakaja na makubaliano,” akasema katika Shule ya Msingi ya Ngukuni, Kaunti ya Makueni ambapo alikuwa ameenda kusimamia uchaguzi wa maafisa wa KNUT katika tawi la eneo hilo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa KUPPET, Bw Akelo Misori, alipuuzilia mbali matamshi hayo ya Bw Oyuu na kusema si kweli kwamba KUPPET inatumiwa na serikali kulemaza juhudi za walimu kupigania haki zao.

Kulingana na Bw Misori, KNUT ndiyo inakosea kwa kutokuwa na mipango bora kuhusu jinsi ya kushauriana na serikali.

“Walijua kwamba mgomo haungefanikiwa ndiposa wakaanza kutoa miito isiyo na msingi,” akasema, huku akitetea jinsi chama chake kilivyokubaliana na serikali kwa haraka.

“Mashauriano kati yetu na TSC yalikuwa kwa msingi wa mapendekezo yetu kuhusu njia bora ya kutatua masuala tatanishi kwenye makubaliano ya pamoja, na mkutano wetu ulikuwa mfupi kwa sababu tu hodari katika kueleza kile kinachohitajika kufanywa,” akasema.

Tofauti na KNUT ambayo imekuwa ikitoa wito wazi kutaka uhamisho wa walimu usitishwe, KUPPET imekuwa ikitoa wito walimu wapewe marupurupu ya kufanya kazi katika maeneo ya mbali, na pia urekebishaji wa viwango vya marupurupu ya kodi ya nyumba bila kujali eneo ambako walimu wanaishi.

Kulingana na Bw Misori, walimu watakubali mpango wa kuhamishwa kutoka maeneo ya jamii zao ikiwa serikali itawalipa marupurupu hayo yaliyopendekezwa.