Knut yakosoa serikali kurukia Gredi ya 7, 8 na 9

Knut yakosoa serikali kurukia Gredi ya 7, 8 na 9

NA TITUS OMINDE

WANAFUNZI wa Sekondari Msingi wanapojiunga na Gredi ya saba kote nchini leo Jumatatu, walimu wameikosoa serikali kwa kuendeleza mfumo ambao utafeli.

Chama cha kitaifa cha Walimu nchini (KNUT) kinasema uamuzi wa serikali kuendeleza mfumo wa CBC bila kuwepo matayarisho ya kutosha, si tu hatari kwa mustakbali wa watoto nchini, bali unaonyesha wanaounda sera hawajali kuhusu iwapo mfumo huu utafaulu au la.

Katibu mtendaji wa tawi la Trans Nzoia la chama hicho, Bw George Simiyu, alisema kukosekana kwa walimu wa kutosha wa kufundisha gredi ya Saba, ni ushahidi kuwa serikali inafanya majaribio na maisha ya watoto.

Bw Simiyu alisema kwa sasa serikali imeweka angalau mwalimu mmoja kwa kila shule na hivyo kuwawia vigumu walimu kusimamia wanafunzi wa shule hizo kufundisha katika Sekondari Msingi.

“CBC ni mfumo unaokuza uvumbuzi. Ili uvumbuzi ufaulu, kila mwalimu anapaswa kushughulikia idadi ndogo ya wanafunzi ili kuchochea usikivu wa mtu binafsi ili vipaji viibuliwe. Inashangaza kwamba shule zikifunguliwa serikali itaajiri mwalimu kwa kila shule. Tunajiuliza iwapo mwalimu huyu mmoja ataweza kufundisha masomo yote 14 katika shule ya Sekondari Msingi,” akasema.

Walimu wanaotakiwa kufundisha katika sekondari Msingi wanahitajika kuwa na shahada ya chuo kikuu. Wale waliopo kwa sasa ni walio na P1 na wachache wa diploma.

Walimu

“Iwapo serikali inataka CBC ifaulu, ni lazima iajiri walimu wasiopungua wanane kwa kila shule kufundisha CBC. La sivyo, tutaharibu hatima ya kizazi kizima cha CBC,” akasema Bw Simiyu.

Alikuwa akizungumza katika eneo la Moi’s Bridge wikendi, alipohudhuria mazishi ya mke wa mwalimu kutoka kaunti ya Trans Nzoia.

Bw Simiyu aliyeandamana na mwenyekiti wa tawi hilo, Bw Wilberforce Wamalwa, alisikitika kwamba serikali ilikosa kuzingatia ushauri wa Knut wakati wa uongozi wa aliyekuwa katibu Mkuu Bw Wilson Sossion.

Mbunge huyo maalumu wa zamani wa ODM, alikuwa ameishauri serikali icheleweshe utekelezaji wa mfumo wa CBC, hadi wakati ambapo nchi ingeweka miundomsingi inayohitajika, pamoja na rasilimali za kushughulikia mtaala husika.

Bw Simiyu alisema kwa kuwa ushauri huo wa awali ulipuuzwa, kilichosalia sasa ni kwa serikali kuajiri walimu wasiopungua wanane kwa kila shule. Alisema ni kwa kufanya hivyo tu ambapo masomo 14 kwa Sekondari Msingi yatasomeshwa kikamilifu.

Bw Wamalwa kwa upande wake alisema hata wazazi wa Sekondari Msingi hawako tayari kwa mfumo huo.

Alisema kuwa wazazi watalazimika kuingia zaidi mifukoni mwao kufanikisha mfumo huo, kwani watalazimika kuchangia ujenzi wa miundo msingi katika shule zao.

“Ninawahurumia wazazi kwa kuwa watalazimika kulipa karo ya ziada kuanzia kwa ununuzi wa sare mpya. Kuna ujenzi wa madarasa, maabara kati mwa miundombinu mingine,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto kuzuru Pwani tena siasa ikizidi kurindima

Leicester wasuka upya safu yao ya uvamizi kwa kusajili...

T L