Habari Mseto

KNUT yalaumu wanasiasa kuchochea uvamizi wa walimu shuleni 

January 22nd, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

MUUNGANO wa kutetea walimu nchini (KNUT) tawi la Pokot Magharibi umeungana na wanaharakati wenza katika sekta ya elimu kukashifu vikali visa vya walimu kushambuliwa kwa madai ya wanafunzi kupata matokeo duni.

Maafisa wa KNUT Pokot Magharibi, wameongeza sauti yao katika malalamishi ya walimu siku chache baada ya shule mbili za upili Eneo la Magharibi mwa Kenya na Bonde la Ufa), kuvamiwa na wazazi na wanafunzi baada ya kuandikisha matokeo duni katika Mtihani wa Kitaifa Kidato cha Nne (KCSE) 2023.

Shule hizo ni St. Gabriel Isongo (Kakamega) na Mafuta (Uasin Gishu), ambapo wazazi na wanajamii ‘walikamata’ walimu wakuu na kuwatembeza katika kile kilifasiriwa kama adhabu kwa sababu ya matokeo duni ya shule wanazoongoza.

Waziri wa Elimu, Bw Ezekiel Machogu alitoa matokeo rasmi ya mtihani huo Februari 2024.

Tawi la KNUT Pokot Magharibi, limetaja uvamizi wa walimu shuleni kama hatua ya kukosa heshima.

Soma pia https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kaunti/knut-yapendekeza-walimu-baringo-wajihami-kwa-silaha-kukabili-majangili

Katibu wa muungano huo katika kaunti, Martin Sembelo, anasema ni jambo la kuvunja moyo walimu kulaumiwa kutokana na matokeo duni ya mitihani.

Alisisitiza kuwa walimu hutekeleza jukumu lao vyema, na kwamba hawafai kulaumiwa kutokana na uzembe wa wanafunzi.

Akirejelea visa vya majuzi walimu kushambuliwa, Bw Sembelo hata hivyo, alisema baadhi ya matukio hayo yanachochewa na viongozi wa kisiasa.

“Mtihani ni mtandao wenye wahusika wengi, si walimu pekee wanaoshiriki. Na ikiwa kuna matokeao duni, hakuna haja ya kuvamia shule,” alisema Bw Sembelo.

KNUT inataka hatua kali kisheria kuchukuliwa dhidi ya wazazi na wahusika waliovamia shule zilizoathirika.

Bw Sembelo ameitaka Idara ya Polisi (NPS), kupitia kitengo cha uhalifu na jinai (DCI) kufanya uchunguzi wa kina na kufungulia mashtaka walioshambulia walimu.

“Tunahitaji suluhu ya kudumu, na hatutaruhusu vitendo vya aina hiyo,” afisa huyo akasisitiza.

Kuboresha matokeo, Bw Sembelo anapendekeza mazungumzo kuhusu njia mwafaka wanafunzi kupata alama bora, hatua anayosema inahusisha wadauhusika wote, wakiwemo walimu, wazazi na usimamizi wa shule.

Shule zilizoathirika Uasin Gishu na Kakamega, Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) iliondoa walimu wake jambo ambalo linahatarisha mustakabali wa shule hizo kielimu.