Knut yasaka pesa za kuandaa kongamano la wajumbe

Knut yasaka pesa za kuandaa kongamano la wajumbe

Na VITALIS KIMUTAI

CHAMA cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kinatafuta pesa za kuandaa kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) ili kuchagua viongozi wake wapya.

Kulingana na notisi iliyotolewa na chama hicho, wajumbe hao watakutana baada ya miezi miwili kuchagua wanachama wa Kamati Shikilizi ya Kitaifa (NSC) na Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC).

Hata hivyo, chama hicho, kinachozongwa na changamoto nyingi za kifedha, hakijatangaza tarehe na mahala ambapo chaguzi hizo zitafanyika.

Katibu Mkuu Wilson Sossion alisema kongamano hilo litafanyika kutimiza hitaji la taarifa kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi iliyotolewa mnamo Septemba 25 mwaka jana.

“Wakati huu tunakabiliwa na shida kubwa ya kifedha baada ya Tume ya Huduma za Walimu (TSC) na serikali kuzima mfumo ambapo michango ya wanachama ilikuwa ikikatwa moja kwa moja kutoka kwenye mishahara yao na kutumwa kwa akaunti zetu.”

“Hata hivyo, tunashirikiana na washirika wetu kimataifa na humu nchini ili kupata rasilimali za kutuwezesha kufanikisha kongamano la ADC,” akasema Bw Sossion katika taarifa aliyoitoa Aprili 22,2021.

Alisema wajumbe watafahamishwa kuhusu tarehe na mahala pa kongamano hilo “hivi karibuni.”

Bw Sossion, ambaye pia ni mbunge maalum, aliongeza hivi: “Notisi hii imetolewa ili kuwezesha matawi kujiandaa kwa ADC na asasi zote za Knut zishirikiane kuhakikisha kuwa kongamano hilo linafanyika.”

Matawi yote 110 kote nchini yameshauriwa kuandaa mikutano ya kuteua wajumbe watakaoshiriki katika kongamamo hilo.

You can share this post!

Kilio serikali za kaunti zikikosa kulipa mishahara

Nyoro, Wamatangi walaumiana kuhu utafunaji wa pesa za corona