Habari Mseto

Knut yatetea walimu kukiwa na madai wanaamuru watoto wasio na uwezo kifedha kurejea nyumbani

January 21st, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

CHAMA cha kueteta masilahi ya walimu nchini (Knut) umesimama kidete na walimu wake dhidi ya madai kuwa wanawarejesha nyumbani wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza na wasio na uwezo kifedha kugharamia karo na mahitaji yanayotakikana shuleni.

Knut aidha imesema hizo ni tetesi “zinazolenga kuharibia walimu wetu jina” na kwamba wazazi wana sababu zao binafsi kuchelewesha wanao. Hii ni kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane, KCPE 2019, kusemekana kuwa nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa fehda.

Katibu mkuu wa Knut Wilson Sossion alisema Jumatatu wazazi wanaendelea kutathmini iwapo watoto wao watajiunga na shule walizoitwa.

“Sababu hasa ya asilimia 40 ya watahiniwa kukosa kuripoti shuleni, ni wazazi wao kutathmini ikiwa watajiunga na shule walizoitwa. Hakuna mwalimu aliyeamuru mwanafunzi yeyote arejee nyumbani kwa ukosefu wa karo,” akasema Bw Sossion ambaye pia ni mbunge maalum.

Wanafunzi walianza kujiunga na kidato cha kwanza wiki iliyopita, na visa vya wengi wao kukosa kuripoti vimeripotiwa, ukosefu wa uwezo kifedha ukitajwa kama kiini kikuu. Baadhi ya wazazi sehemu mbalimbali nchini wamejitokeza na kujieleza kwamba hana uwezo, licha ya serikali kudai inagharamia kiasi fulani cha karo.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha aliongoza operesheni ya nyumba kwa nyumba katika kile kilionekana kama kuhakikisha watahiniwa wote waliofanya KCPE 2019 wanajiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, 2020.

Ni katika mojawapo ya operesheni Nairobi ambapo Prof Magoha alipigia mzazi mmoja simu hadharani akitaka kujua bayana sababu za mwanawe kukosa kuripoti shuleni.

Serikali imesisitiza kwamba sharti wanafunzi wote waliofanya KCPE 2019, wajiunge na kidato cha kwanza. Aidha, inasema mfumo wa asilimia 100 kwa 100 wa watahiniwa wa KCPE kujiunga na shule za upili lazima uafikiwe.

Rais Uhuru Kenyatta aliibuka na wazo hilo baada ya kuchaguliwa 2017 kuhudumu awamu yake ya pili na ya mwisho.

Licha ya serikali kudai masomo ya shule za msingi na za upili za umma hayana malipo, wazazi wanaendelea kulalamikia kutozwa karo ghali.