Habari Mseto

KNUT yaungana na COTU, lengo si kushinikiza serikali, asema Sossion

January 24th, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

VIONGOZI wa Muungano wa kitaifa wa vyama vya wafanyakazi Kenya (COTU) na Chama cha kitaifa cha kutetea walimu nchini (KNUT) Alhamisi walisema kwamba serikali haifai kuhofia ushirikiano mpya kati yao uliozinduliwa katika jengo la Solidarity jijini Nairobi.

Uongozi wa COTU na KNUT ulisema ushirikiano huo unalenga kumnufaisha mfanyakazi wala hawana lengo la kuzidisha makabiliano dhidi ya serikali wanapowatetea wafanyakazi nchini.

KNUT ilijiunga tena kama mwanachama wa COTU baada ya kuwa nje kwa miaka sita, uamuzi ulioidhinishwa wakati wa mkutano wa wajumbe wa chama hicho mwezi uliopita jijini Nairobi.

Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli na mwenzake wa KNUT Wilson Sossion waliwaongoza wanachama wao kusaini vyeti vya kurasimisha ushirikiano huo na kufikisha idadi ya wanachama wa COTU hadi zaidi ya watu milioni tatu.

“Hatua yetu ya kuungana si mbinu ya kujiandaa kuipiga vita serikali kuhusiana na haki za wafanyakazi nchini. Tumeamua kurejea tena katika COTU ili kuimarisha na kuipa nguvu muungano huu mkubwa zaidi wa wafanyakazi nchini.”

“Sisi tumejiunga na COTU ili kupigania maendeleo ya kiuchumi. Tutaendelea kupigania haki za walimu na hatua hii itatupa nguvu ya kuongeza utetezi ili kuhakikisha serikali inawaheshimu walimu na kuridhia matakwa yao,” akasema Bw Sossion.

Kwa upande wake, Bw Atwoli alisifu hatua waliyoichukua KNUT na kuahidi kwamba watasalia chama huru wala COTU haitaingilia masuala yake ya ndani au kudhamini vita vya ndani ili kuisambaratisha jinsi inavyofanyika katika miungano mingine.

“Nawashukuru sana wajumbe wenu kwa kuridhia hatua mliyoichukua leo. Kujiunga kwenu kunazidisha idadi ya vyama vilivyojiunga na COTU hadi 25 na kuongeza uanachama wetu hadi zaidi ya milioni tatu.”

“Hali ya baadaye ya taifa hili linawategemea wafanyakazi na tutafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba haki zao zinaheshimiwa. Pia mnaruhusiwa kutumia vifaa vyetu kama Taasisi ya Mafunzo ya Wafanyakazi ya Tom Mboya kuwatia makali wanachama wenu,” akasema Bw Atwoli.

Kiongozi huyo pia aliishutumu Tume ya kuwaajiri walimu nchini (TSC) kwa kutotilia manani malalamishi ya walimu yanayowasilishwa kwake kila mara na KNUT na kuiahidi kivumbi kikali huku akisema vita dhidi ya TSC sasa zinahusisha hata COTU.

“Tunaitaka TSC kujiunga na Muungano wa waajiri nchini (FKE) mara moja ili kufahamu namna masuala yanayohusu waajiriwa yanavyo shughulikiwa na waajiri. Iwapo haitafanya hivyo basi itapitwa na wakati na umuhimu wake hautaonekana,” akaongeza Bw Atwoli.

Aidha alifichua kwamba viongozi wa COTU wanalenga kukutana na Rais Uhuru Kenyatta ili kumshawishi kufanya mabadilko katika Tume ya kudhibiti mishara nchini (SRC) baada ya tume hiyo kuwasilisha kesi dhidi ya wafanyakazi mahakamani ingawa hilo si jukumu lake kisheria.