Michezo

Kobala Girls mabingwa wa Kobala Open

January 29th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

KIKOSI cha soka cha timu ya wasichana ya Kobala ndio mabingwa wa Makala ya tano ya Kobala Open Tournament iliyogaragazwa kwenye uga wa shule hiyo inayopatikana katika wadi ya Wang’chieng’, Kaunti ya Homa Bay.

Vipusa hao, ambao ni wapambe wa soka ya ukanda wa Nyanza, waliwalaza wapinzani wao, shule ya msingi ya Kobala mabao 3-0 kwenye fainali kali iliyohudhuriwa na halaiki ya mashabiki siku ya Jumapili Januari 27.

Wanadimba Catherine Adhiambo, Sarah Idzah na Sharon Adongo waliounga na kukamilisha kikosi kilichotinga robo fainali ya mechi za kitaifa za shule za upili mwaka wa 2018 mjini Eldoret ndio walikuwa wafungaji wa mabao hayo matatu.

Katika kitengo cha soka ya wanaume, Shule ya upili ya Simbi waliwapiku waliokuwa mabingwa wa taji hilo, Oriwo Boys’ kupitia bao lake Mark Agu na kushinda taji hilo.

Shule ya mseto ya Kandiege na Kobala Girls nazo zilishinda vitengo vya mpira wa voliboli na kikapu mtawalia. Washindi walipokezwa zawadi kochokocho pamoja na kombe, mipira na medali ya kipekee.

Vipusa wa Kobala wakichuana na Sophia Queens kwenye mchezo wa vikapu wakati wa makala ya tano ya mashindano ya Kobala Open Tournament. Picha/ Cecil Odongo

Mratibu wa mashindano hayo George Adoyo anayesimia idara ya michezo katika shule ya Kobala, alitoa wito kwa wafadhili wajitokeze na kutoa udhamini wao kwa makala ya mwaka wa 2020 ili kulipiga jeki lengo lao la kukuza na kulea vipaji.

“Tunawaomba wadhamini waje ili tufanikishe makala ya mwaka ujao na pia kukuza ukwasi wa talanta unaopatikana eneo hili. Pia tunatoa wito kwa timu zinazoshiriki ligi mbalimbali nchini wafike hapa ili kujionea na kuwasajili baadhi ya wanasoka wetu ambao nina hakika watawatambisha kwenye ligi hizo,” akasema Bw Adoyo.

c
Kikosi cha wanasoka wa Shule ya upili ya Simbi wakati wa Kobala Open Tournament katika Shule ya upili ya Kobala. Picha/ Cecil Odongo