Habari

Kobia alimteka nyara na kumtesa raia wa Congo kwa bunduki, mahakama yaambiwa

June 7th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Congo aliyedaiwa kumlaghai mfanyabiashara maarufu wa humu nchini Bw Paul Kobia Sh40 milioni akidai angemuuzia madini alitumia gari lake muundo wa Mercedez Benz kujikomboa baada ya kutekwa nyara na kuteswa, afisa mkuu wa polisi aliambia mahakama Alhamisi.

Inspekta Joseph Kituyi alimweleza hakimu mkuu Bw Francis Andayi kuwa Bw Kobia (pichani juu) alimteka nyara na kumtesa Bw Londole Iseka Blanchard kutoka kilabu cha Boston kilichoko eneo la Kilimani, Nairobi na kumzuilia nyumbani kwake mtaani Kileleshwa.

Inspekta Kituyi alisema alifika nyumbani kwa Bw Kobia mwendo wa saa nane unusu usiku wa manane na kumpata Londole amelala kwenye sakafu akilia huku mshtakiwa akiteta kwa ghadhabu akisema, “Mtu hawezi kunipora Sh40 milioni na kuzitumia kuninyang’anya mke wangu.”

Akitoa ushahidi, Inspekta Kituyi alisema aliandamana katika oparesheni hiyo na Sajini Hellen Wambui aliyemjulisha kuhusu kutekwa nyara kwa Londole na wanaume watano.

“Sajini Wambui alinipigia simu nikiwa kwenye doria na kunieleza amejulishwa raia wa Congo alitekwa nyara kutoka kilabu cha Boston na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki,” alisema Insp Kituyi.

Hakimu alijulishwa Bw Kobia alienda kwenye kilabu hicho kinachomilikiwa na Bi Irene Bambashi na kumpata Londole mle ndani.

Paul Kobia akiwa kizimbani Juni 7, 2018 kwa kosa la kufyatua bunduki hadharani kutisha umma na kumteka nyara raia wa Congo jijini Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Risasi ya kutisha

“Bw Kobia ambaye ni mteja kwenye kilabu hicho alitoka nje alipomwona Londole na kurudi tena akiwa amejihami na bunduki. Alikuwa ameandamana na wanaume watano waliokuwa wamejikwatua suti nyeusi. Aliwaamuru wamshike Londole. Alipodinda kuandamana nao Bw Kobia alifyatua risasi ya kutisha ndipo Londole akakubali kuandamana nao,” Insp Kituyi alidokeza.

Hakimu alifahamishwa kuwa Londole aliingizwa kwenye gari jeusi muundo wa Range Rover kisha ikachomoka kama mshale.

Afisa huyo wa polisi alisema kisa hicho kiliripoptiwa katika kituo cha Polisi cha Kilimani kwa njia ya simu na Bi Irene Bambashi.

Mwenye kupokea simu hiyo alikuwa Sajini Wambui ambaye alimjulisha Insp Kituyi.

Habari za kutekwa nyara kwa Londole zilisambazwa kwa vituo vyote jijini na kwa maafisa wote wa polisi waliokuwa wanashika doria usiku huo wa Machi 9 2017.

“Tulifahamishwa kuwa Bw Kobia ndiye alimteka nyara Londole. Tulipelekwa kwa Bw Kobia usiku huo kisha nikabisha. Lango lilikuwa limefungwa lakini kulikuwa na watu ndani wakiongea,” Bw Andayi alifahamishwa.

Hakimu aliambiwa Bw Kobia alitoka kufungua lango mwenyewe.

“Kobia aliinua mikono alipokuta sisi ni maafisa wa polisi. Alituelekeza ndani ndipo tukampata Londole akiwa amelala chini akilia huku akiwa na majeraha,” Insp Kituyi alisema.

Bunduki inayomilikiwa na Paul Kobia pamoja na bahasha yenye risasi zilipowasilishwa kortini kama ushahidi Juni 7, 2018. Picha/ Richard Munguti

Bunduki kwa kiti

Alisema walipekua nyumba hiyo na kupata alikuwa ameificha bunduki kwenye kiti cha sofa na wanaume wanne waliokuwa wamejikwatua Suti nyeusi kila mmoja wamejificha kwa choo.

Mahakama iliambiwa kwenye eneo la egesho kulikuwa na Range Rover KBY 506Y (rangi nyeusi) na Mercedez nambari ya usajili KCK 306H.

Baada ya kumhoji Londole alisema “alikuwa amempa Bw Kobia Mercedez yake ajinusuru.”

“Je ,kulikuwa na ripoti yoyote ya Bw Kobia kwamba alikuwa ametapeliwa Sh40 milioni na Londole?” kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimwuliza Insp Kituyi

“La,” alijibu.

“Je, wakati Bw Kobia alimshika Londole alimpeleka kituo cha polisi au la?” akauliza Naulikha

“La. Alimpeleka nyumbani kwake ambapo sio Kituo cha Polisi,” alijibu Insp Kituyi.

Wakili Kirathe Wandugi (kushoto ) akimhoji Sajini Helllen Wambui kuhusu bunduki ya Paul Kobia kutummika kumtesa raia wa Congo. Picha/ Richard Munguti

Sajini Wambui na Insp Kituyi walimtambua Bw Kobia kortini kama mtu yule aliyemteka nyara Londole na kupatikana na bunduki. Bunduki hiyo na risasi nne zilitolewa kortini kuwa ushahidi.

Wakili Kirathe Wandugi anayemwakilisha Bw Kobia aliambia kortini  mshtakiwa alipeleka leseni ya umiliki wa bunduki hiyo kwa polisi.

Maafisa hao wa polisi walitoa bunduki hiyo kama ushahidi pamoja na risasi nne na ganda moja.

Bw Kobia anashtakiwa kwa kuwa na utundu hadharani wa kubeba bunduki. Yuko nje kwa dhamana. Kesi iliahirishwa. Mashahidi watatu watatoa ushahidi kesi ikisikizwa tena.