Michezo

Kocha afutwa Valencia, naye mkurugenzi wa spoti ajiuzulu

June 30th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KLABU ya Valencia imemfuta kazi kocha Albert Celades baada ya kudhibiti mikoba yao kwa kipindi cha miezi tisa pekee.

Kutimuliwa kwa Celades kunajiri saa chache baada ya kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kuagana pia na mkurugenzi wa spoti, Cesar Sanchez aliyejiuzulu.

Voro Gonzalez kwa sasa anajeza pengo la Celades hadi mwishoni mwa kampeni za msimu huu.

Hii ni mara ya sita kwa Gonzalez ambaye amekuwa kocha msaidizi kuwa mkufunzi mshikilizi wa mikoba ya kikosi cha Valencia.

Gonzalez alipokezwa mikoba ya Valencia kwa muda mnamo 2008 baada ya klabu hiyo kumfurusha kocha Ronald Koeman.

Chini ya uongozi wake, Valencia waliponea chupuchupu kukabiliwa na shoka ambalo vinginevyo, lingewashuhudia wakiteremshwa ngazi kwenye La Liga.

Celades aliteuliwa kuwa kocha wa Valencia mnamo Septemba 2019 baada ya kutimuliwa kwa Marcelino Garcia Toral.

Anakuwa mkufunzi wa sita kufurushwa na Valencia tangu bilinonea mzawa wa Singapore, Peter Lim atwae umiliki wa kikosi hicho mnamo 2014.

Aidha, Sanchez ambaye aliajiriwa na Valencia mnamo Januari 2020 anakuwa mkurugenzi wa spoti wa sita kujiuzulu kambini mwa kikosi hicho chini ya kipindi cha miaka sita iliyopita.

Celades anaondoka Valencia baada ya Sanchez kujiuzulu mnamo Juni 29, 2020, alipowahakikishia wachezaji kwamba hatakuwa sehemu ya benchi ya kiufundi itakayowaongoza kuvaana na Athletic Bilbao katika gozi la La Liga mnamo Jumatano ya Julai 1, 2020.

Kufikia sasa, Valencia wamepoteza mechi tatu kati ya nne zilizopita ligini.

Wanashikilia nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama 46, nane nyuma ya Sevilla wanaofunga mduara wa nne-bora kileleni.