Michezo

Kocha amsifu kinda kwa weledi wa soka

July 18th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI  wa Mathare United Francis Kimanzi amemsifu chipukizi Klinsman Omulanga baada ya kinda huyo kufunga bao safi kwenye sare ya  3-3 waliosajili dhidi ya Wazito FC kwenye mechi ya ligi ya KPL iliyosakatwa Jumamosi 14 uwanjani Kenyatta, Kaunti ya Machakos.

Omulanga ambaye alijiunga na mabingwa hao wa mwaka 2008 kutoka Liberty Academy alionyesha umahiri wake baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba na kuonyesha kiwango cha juu cha usakataji kabumbu.

“Ameonyesha weledi wake kwenye mazoezi kwa muda wa wiki mbili zilizopita na sisi pamoja na benchi ya kiufundi tuliamua kwamba atajumuishwa kwenye mechi hii na zile zijazo, nafurahi kwamba alifanya kweli katika mechi ya leo,” akasema Bw Kimanzi.

Mathare United walilazimika kutoka nyuma na kusajili sare hiyo dhidi ya Wazito FC  wanaokodolewa macho na shoka la kuwashusha ngazi.