Michezo

Kocha ashangaa ligi ya mabinti kuwa na ushindani mkali

May 22nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KOCHA mkuu wa Uweza Women, Charles ‘Stam’ Kaindi amekiri wazi kwamba kivumbi cha kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) kinashuhudia upinzani mkali msimu huu.

Kaindi amesema hayo licha ya  kikosi chake kitazidi kupigana kwa udi na uvumba kutafuta kumaliza kileleni na kupata tiketi ya kushiriki ‘play off’ ya kupigania nafasi ya kufuzu kupandishwa ngazi msimu ujao.

Alisema hayo baada ya wasichana hao, Uweza Women kuteleza na kutoka sare ya mabao 2-2 na Amani Queens.

Kwenye matokeo mengine Fasila ‘Kamama’ Adhiambo alipiga ‘hat trick’ naye Damaris Akinyi alichapa moja safi na kubeba Kangemi Ladies kutwaa mabao 4-0 mbele ya City Queens kwenye mechi ya iliyosakatiwa uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

”Sina budi kupongeza wasichana wangu kwa jitihada zao maana tunataka kuibuka mabingwa ingawa tunafahamu tuna shughuli zito mbele ya mahasimu wetu,” kocha wa Kangemi Ladies, Loice Karanja alisema. Ni matamshi yaliyoungwa na mkono na bosi wa Amani Queens, Ben Ooko alipotaja kuwa kampeni za msimu huu zinazidi kushuhudia ushindani mkali.

Kwenye patashika ya kikosi chake, Joan makobe na Lydia Ali kila mmoja alipiga moja safi nao Mildred Hanisi na Gentrix Murunda walitingia Uweza Women bao moja kila mmoja.

Mechi zingine, Kibagare Girls iliikomoa The UoN Queens mabao 2-0 nao warembo wa Lifting The Bar walitoka sare tasa na Carolina for Kibera. Matokeo hayo yalifanya Kangemi Ladies kurukia usukani wa kipute hicho kwa kufikisha alama 14 sawa na Uweza Women tofauti ikiwa idadi ya mabao.