Michezo

Kocha awasifu vijana wake kukomoa Spurs

March 12th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

BERLIN, Ujerumani

KOCHA Julian Nagelsmann wa klabu ya RB Leipzip amesema amefurahia ushindi wa 3-0 dhidi ya Tottenham Hotspur ambao umewezesha vijana wake kusonga mbele katika michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

Klabu hiyo ya Ujerumani iliyobuniwa miaka 10 iliyopita, ilianza mechi hiyo ikiwa kifua mbele baada ya ushindi wa 1-0 wa pambano la mkondo wa kwanza.

Wenyeji walijipatia mabao mawili ya haraka kupitia kwa Marcel Sabitzer katika mechi hiyo ya raundi ya 16 bora iliyochezewa Red Bull Arena.

Kipa Hugo Lloris atalaumiwa kwa mabao yote mawili kwa vile alikuwa na uwezo wa kuyaokoa. Bao la tatu lilifungwa na Emil Forsberg alilofunga mara tu alipoingia.

Spurs ambao wanakabiliwa na majeraha mengi kwa wachezaji wao muhimu walionekana kulemewa kwenye mechi hiyo.

Vijana hao wa kocha Jose Mourinho- ambao hawajapata ushindi katika mechi sita za mashindano tofauti, itabidi watafute mbinu mpya za kuwawezesha kurejea katika mashindano haya msimu ujao.

Hata hivyo, haitakuwa rahisi kwa vile wako nyuma kwa mwanya wa pointi saba dhidi ya Chelsea wanaoshikilia nafasi ya nne katika msimamo wa EPL.

Mourinho aliwekewa matumaini makubwa ya kuiongoza Spurs kupiga hatua kubwa baada ya kuongoza FC Porto na Inter Milan kutwaa ubingwa huo wa Ulaya mnamo 2004 na 2010 mtawaliwa, lakini mambo yanaonekana kwenda mrama.

Kocha huyo ameshindwa kutwaa taji lolote tangu 2014 akiwa kwenye usukani katika mechi 935.

Mourinho amejitetea kwamba kubanduliwa kwa kikosi chake kumetokana na kuumia kwa baadhi ya nyota wake, wakiwemo Steven Bergjijn, Harry Kane, Son Heung-min na Moussa Sissoko.

Leipzig walionekana kuwa na tamaa, hasa katika kipindi cha kwanza, huku wakiwaacha wachezaji wa Spurs kuonekana wanafunzi wa soka.

Kiungo mahiri Timo Werner aliyefunga bao la ushindi katika mkondo wa kwanza alionekana kumlemea Eric Dier, huku Angelino alimsumbua beki Serge Aurier mara kwa mara.

Tangu ibuniwe mnamo 2009, Leipzig imepanda ngazi mara nne na kufuzu kwa fainali ya German Cup. Lakini ilikuwa mara yao ya kwanza ya kushiriki katika michuano hiyo ya maondoano.