Michezo

Kocha awataka wachezaji wapya kikosini wapiganie nafasi katika timu

March 12th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Gor Mahia Steven Polack amewataka wachezaji wapya ambao walisajiliwa na timu hiyo wapiganie nafasi yao katika timu, huku mbio za kuwania taji la Ligi Kuu (KPL) zikiwa kwenye mkondo wa lala salama.

K’Ogalo ambao ni mabingwa watetezi wapo kileleni mwa msimamo wa jedwali la KPL kwa alama 54, saba mbele ya Kakamega Homeboyz ambayo bado ina mechi moja zaidi ya kuwajibikia huku zikiwa zimesalia mechi tisa kabla ya msimu wa 2019/20 kutamatika.

Baadhi ya wachezaji waliosajiliwa na Gor mnamo Januari ni raia wa Uganda Juma Balinya, Mghana Jackson Owusu, Clinton Okoth na Nicholas Omondi.

Owusu alisajiliwa kutoka Asante Kotoko ambako Polack alikuwa akifunza kuhusu soka kabla ya kujiunga na K’Ogalo na amekuwa akipangwa katika kikosi cha kwanza ikiwemo ushindi 1-0 dhidi ya AFC Leopards kwenye debi ya Mashemeji Jumapili iliyopita.

Balinya ambaye alisajiliwa kutoka Yanga SC kama mrithi wa mshambulizi wembe wa Ivory Coast, Yikpe Ghislain naye alianza mechi yake ya kwanza kwa matao ya juu Februari.

Alifunga mabao mawili walipokutana na Nzoia Sugar lakini amekuwa akilishwa benchi huku Nicholas Kipkirui akitwikwa jukumu la kuongoza safu ya ushambulizi ya K’Ogalo.

Kabla ya kujiunga na Gor, Okoth alikuwa mfungaji bora kwenye Ligi ya Supa kwa mabao 14 akiwajibikia Migori Youth. Omondi naye alikuwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha Kibera Black Stars ambayo pia inashiriki NSL.

Polack alisema Okoth na Omondi wamekuwa wakikosa mechi za KPL kwa sababu bado hawajaiva kucheza kwenye ligi hiyo.

“Chipukizi hao hawajakuwa kwa kikosi kwa sababu bado hawajaiva kushiriki KPL na sidhani kama watacheza kabla ya mechi za ligi kukamilika. Sijakuwa nikiwaacha nje kimakusudi bali mimi humpanga mchezaji kikosini kutokana na jinsi anavyoridhisha mazoezini,” akasema Polack.

Kauli ya Polack inajiri baada ya tetesi kuzuka kwamba ameamua kutowajibisha uwanjani, Balinya, Omondi na Okoth akidai walisajiliwa bila idhini yake wakati wa uhamisho wa Januari.

Inadaiwa kwamba hatua ya kocha huyo kuwapuuza watatu hao kumewachemsha nyongo uongozi wa klabu hiyo ambao unadai kwamba nia yake ni kusambaratisha taaluma yao ya soka.

Mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier pamoja na maafisa wengine wa klabu inasemekana waliandaa mkutano na raia huyo wa Uingereza kuhusu kupuuzwa kwa wanasoka hao.

“Aliamrishwa afike afisini mwa mwenyekiti ambapo alielezwa asiwabague wachezaji hao na badala yake awajumuishe kikosini. Anafaa akome kuwahukumu kwa sababu tu ya kutowasajili au kutohusishwa kwenye mchakato wa kusajiliwa kwao,” akasema mmoja wa maafisa ambaye hakutaka anukuliwe.

Akiongea na ‘Taifa Leo’, Polack alikiri mkutano huo ulifanyika.