Kocha Benitez pazuri zaidi kuwa mrithi wa Ancelotti kambini mwa Everton

Kocha Benitez pazuri zaidi kuwa mrithi wa Ancelotti kambini mwa Everton

Na MASHIRIKA

KOCHA Rafael Benitez yuko pua na mdomo kupokezwa mikoba ya kikosi cha Everton kinachotafuta mrithi wa mkufunzi Carlo Ancelotti aliyeagana nao ghafla mwanzoni mwa Juni 2021 na kurejea kambini mwa Real Madrid, Uhispania.

Kwa mujibu wa gazeti la Mirror Sport nchini Uingereza, mazungumzo kati ya Benitez na vinara wa Everton yamefikia hatua muhimu zaidi na dalili zote zinaashiria kwamba ndiye atakayeajiriwa na kikosi hicho kilichokamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2020-21 katika nafasi ya 10 jedwalini.

Nuno Espirito Santo aliyekatiza uhusiano wake na Wolves mwishoni mwa msimu wa 2020-21 amekuwa pia akihusishwa na mikoba ya Everton.

Hata hivyo, tajriba ya Benitez ambaye pia amewahi kuwanoa Liverpool, Chelsea, Real Madrid, Newcastle United na Dalian Professional ya China inamweka pazuri zaidi kuteuliwa. Benitez amewahi pia kuwatia makali vijana wa Valladolid, Osasuna, Valencia, Inter Milan na Napoli.

Iwapo mpango wake wa kutua ugani Goodison Park utafaulu, basi ataweka historia ya kuwa kocha wa kwanza kuwahi kudhibiti mikoba ya vikosi viwili vya Merseyside – Everton na Liverpool aliowashindia taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Kombe la FA katika kipindi cha miaka sita ya kuhudumu kwake ugani Anfield kati ya 2004 na 2010.

Benitez aliwahi kuwakera mashabiki wengi wa Everton kwa kuita klabu hiyo “kikosi kidogo sana” baada ya masogora wake wa Liverpool kulazimishiwa sare katika mechi ya EPL mnamo Februari 2007.

Kuajiriwa kwake pia na Chelsea mnamo Novemba 2012 hakukupokelewa vyema na mashabiki wa kikosi hicho ikizingatiwa uhasama mkubwa kati ya The Blues na Liverpool wakati huo. Hata hivyo, Benitez ambaye ni raia wa Uhispania, aliongoza Chelsea kutinga nafasi ya tatu kwenye jedwali la EPL mwishoni mwa msimu na akawanyanyulia taji la Europa League.

Kikosi cha mwisho kwa Benitez kunoa katika EPL ni Newcastle kilichojivunia maarifa yake kati ya 2016 na 2019 kabla ya kuhamia China kudhibiti mikoba ya Dalian Professional kwa msimu mmoja.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mabeki Maguire na Tierney kurejea katika vikosi vyao vya...

Man-City kuanza kutetea ubingwa wa EPL kwa kibarua kizito...