Kocha Bielsa ataka Leeds United warefushe mkataba wake huku kikosi hicho cha EPL kikitema wanasoka wawili

Kocha Bielsa ataka Leeds United warefushe mkataba wake huku kikosi hicho cha EPL kikitema wanasoka wawili

Na MASHIRIKA

KOCHA Marcelo Bielsa wa Leeds United ameandaa kikao na waajiri wake akitaka kipindi cha kuhudumu kwake uwanjani Elland Road kurefushwa huku akiwasisitizia kwamba asingetaka kuhamia kwingineko.

Mkufunzi huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 65, amekuwa akidhibiti mikoba ya Leeds United tangu mwaka wa 2018 na alitia saini mkataba mpya saa 24 kabla ya kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kuanza rasmi mnamo Septemba 2020.

Awali, Bielsa aliyerejesha Leeds United kwenye EPL msimu huu baada ya kuwa nje kwa miaka 16, alisema kwamba angeweka wazi kuhusu mustakabali wake katika taaluma ya ukocha baada ya mchuano wa mwisho wa msimu huu dhidi ya West Brom mnamo Mei 23, 2021.

“Maamuzi ya kusalia kambini mwa Leeds United yamekuwa rahisi sana kufikia. Kwa sasa sioni kwingine pa kuwazia kwenda kwa sababu ya ukubwa wa mapenzi yangu kwa kikosi hiki,” akasema.

Leeds wametangaza kwamba wataagana rasmi na wanasoka Pablo Hernandez na Gaetano Berardi mwishoni mwa msimu huu. Wawili hao walichangia pakubwa kupandishwa ngazi kwa Leeds United hadi EPL mnamo 2020-21.

Berardi ambaye ni raia wa Uswisi, ndiye mwanasoka ambaye amehudumu kambini mwa Leeds kwa muda mrefu zaidi tangu asajiliwe na kikosi hicho mnamo 2014.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 alipata jeraha baya la goti mwishoni mwa msimu wa 2019-20 na aliwajibishwa kwa mara ya kwanza msimu huu dhidi ya Southampton mnamo Mei 18 uwanjani St Mary’s.

Kwa upande wake, kiungo Hernandez ambaye ni raia wa Uhispania, amechezea Leeds katika jumla ya michuano 16 muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Beki matata wa Leicester City, Wes Morgan, kustaafu soka...

Gicheru afananisha afisi ya Bensouda na mchawi asiye na...