Michezo

Kocha De Boer ashauri Zirkzee apuuze Man United ajiunge na Arsenal

May 24th, 2024 1 min read

KOCHA wa zamani wa Uholanzi, Frank de Boer ameomba Mholanzi mwenzake Joshua Zirkzee achague Arsenal FC badala ya Manchester United akiamua kuondoka Bologna nchini Italia katika kipindi kirefu cha uhamisho kinachofunguka Juni 14 hadi Septemba 2.

Mshambulizi Zirkzee amechangia pakubwa katika kampeni za Bologna msimu huu, akiisaidia kujikatia tiketi ya kushiriki Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Bologna ya kocha Thiago Motta inakamata nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Italia ikisalia mechi moja msimu ufike kilele.

Zirkzee anaongoza kuifungia mabao baada ya kucheka na nyavu mara 11.

Chipukizi huyo wa zamani wa Bayern Munich alihusishwa na kuingia Ligi Kuu ya Uingereza katika kipindi kifupi cha uhamisho mwezi Januari, lakini akaamua haendi popote.

Bado ana kandarasi na Bologna hadi mwaka 2026, lakini klabu za Uingereza zinatarajiwa kumrushia chambo tena soko litakapofunguliwa.

Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag alilalamika kukosa kusaini mshambulizi Januari kutokana na sheria za faida na uendelevu, lakini kuwasili kwa mmiliki mpya Jim Ratcliffe huenda kukafungulia klabu hiyo milango ya shughuli nyingi sokoni.

Arsenal pia wanamezea mate Zirkzee wakilenga kuimarisha safu ya mashambulizi baada ya kukosa taji pembamba na De Boer amedai itakuwa busara kwake kuhamia ugani Emirates badala ya Old Trafford.