Michezo

Kocha Frank Lampard athibitisha Pedro Rodriguez anayoyomea AS Roma kula Sh7 milioni kwa wiki

July 28th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MECHI iliyowakutanisha Chelsea na Wolves katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Julai 26, 2020 uwanjani Stamford Bridge ndiyo ilikuwa ya mwisho kwa kiungo mvamizi Pedro Rodriguez kusakata akivalia jezi ya ‘The Blues’.

Kocha Frank Lampard amethibitisha kwamba Pedro, 33, ataondoka rasmi uwanjani Stamford Bridge baada ya fainali ya Kombe la FA itakayowakutanisha na Arsenal mnamo Agosti 1, 2020.

Fowadi huyo mzawa wa Uhispania aliwajibishwa kwa dakika chache za mwisho wa kipindi cha pili dhidi ya Wolves.

Pedro aliingia katika sajili rasmi ya Chelsea mnamo 2014 baada ya kuagana na Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa kima cha Sh2.9 bilioni. Tangu wakati huo, amewasaidia Chelsea kunyanyua taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2016-17, taji moja la Europa League na Kombe la FA.

Pedro anahusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua kambini mwa AS Roma inayoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Roma wamefichua kwamba tayari wameagana na Pedro kuhusu uwezekano wa kumsajili kwa mkataba wa miaka miwili huku akitia mfukoni kima cha Sh7 milioni kwa wiki.

Roma watakuwa na fursa ya kurefusha mkataba wa Pedro kwa miezi 12 zaidi mwishoni mwa msimu wa 2022-23. Kandarasi ya Pedro na Chelsea ilitarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa Mei 2020 ila akarefusha zaidi mwanzoni mwa Juni hadi mwisho wa kampeni za msimu huu.

Kuondoka kwa Pedro kutatamatisha kipindi cha miaka mitano ya kuhudumu kwake kambini mwa Chelsea tangu atue jijini London, Uingereza mnamo Agosti 2015 baada ya kuagana rasmi na Barcelona waliompokeza malezi ya soka akiwa mtoto.

Hadi kufikia sasa, Pedro amewafungia Chelsea jumla ya mabao 43 kutokana na mechi 205 na aliwasaidia waajiri wake hao kunyanyua ubingwa wa EPL mnamo 2017, Kombe la FA mnamo 2018 na taji la Europa League mnamo 2019.

Tangu ujio wa kocha Frank Lampard kambini mwa Chelsea mwishoni mwa msimu wa 2018-19, Pedro amewajibishwa mara 22 pekee katika mapambano yote. Katika juhudi za kujaza pengo la Pedro, Chelsea tayari wamejinasia huduma za Hakim Ziyech kutoka Ajax ya Uholanzi na Timo Werner kutoka RB Leipzig nchini Ujerumani.