Kocha Gareth Southgate aita Jarrod Bowen na James Justin kambini mwa Uingereza kwa mara ya kwanza

Kocha Gareth Southgate aita Jarrod Bowen na James Justin kambini mwa Uingereza kwa mara ya kwanza

Na MASHIRIKA

KOCHA Gareth Southgate amejumuisha fowadi Jarrod Bowen wa West Ham United kwa mara ya kwanza katika kikosi chake cha Uingereza kitakachovaana na Hungary, Ujerumani na Italia kwenye michuano ijayo ya Nations League mnamo Juni 2022.

Bowen alifungia West Ham mabao 18 na kuchangia mengine 13 katika kampeni za msimu huu wa 2021-22. Sogora huyo mwenye umri wa miaka 25 alitazamiwa kuwajibishwa kwenye mechi za Uingereza mnamo Machi 2022 ila mpango huo ukatibuliwa na jeraha la mguu.

Beki wa kulia kambini mwa Leicester City, James Justin naye ameitwa katika kikosi cha Uingereza kwa mara ya kwanza huku Fikayo Tomori naye akijumuishwa baada ya kuongoza AC Milan kutwaa taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Kiungo Kalvin Phillips wa Leeds United na beki wa Newcastle United, Kieran Trippier pia wamerejea kambini mwa Uingereza baada ya kupona majeraha.

Nahodha wa Liverpool, Jordan Henderson ameachwa nje ya kikosi baada ya kuhusika pakubwa katika kampeni za waajiri wake msimu huu ambao wataufunga kwa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Real Madrid mnamo Mei 28, 2022 jijini Paris, Ufaransa.

Wachezaji wengine ambao wametupwa nje na Southgate ni beki wa Tottenham Hotspur Eric Dier na Joe Gomez. Hivyo, beki Trent Alexander-Arnold ndiye mchezaji wa pekee wa Liverpool atakayeunga kikosi cha Uingereza.

Beki wa Manchester City, Kyle Walker, ametiwa kikosini mwa Uingereza licha ya kutowajibishwa katika mechi yoyote ya EPL tangu katikati ya Aprili 2022 baada ya kupata jeraha la kifundo cha mguu.

Wachezaji wengine katika kikosi hicho ni Tammy Abraham aliyefungia AS Roma ya kocha Jose Mourinho mabao 27 msimu huu, Dominic Calvert-Lewin wa Everton na mafowadi watatu wa Man-City – Phil Foden, Jack Grealish na Raheem Sterling.

Southgate ametupilia mbali ombi la kocha Mikel Arteta la kutomjumuisha kikosini mwake chipukizi Bukayo Saka, 20, ambaye amehusika katika mchuano uliosakatwa na Arsenal katika EPL mnamo 2021-22.

Jadon Sancho, Marcus Rashford, James Maddison, Tyrick Mitchell, Kyle Walker-Peters, Emile Smith Rowe na Ollie Watkins ni wachezaji wengine ambao wametemwa na Southgate.

KIKOSI CHA UINGEREZA

MAKIPA: Jordan Pickford (Everton), Nick Pope (Burnley), Aaron Ramsdale (Arsenal).

MABEKI: Trent Alexander-Arnold (Liverpool), Conor Coady (Wolves), Marc Guehi (Crystal Palace), Reece James (Chelsea), James Justin (Leicester), Harry Maguire (Man Utd), John Stones (Man City), Fikayo Tomori (AC Milan), Kieran Trippier (Newcastle), Kyle Walker (Man City), Ben White (Arsenal).

VIUNGO: Jude Bellingham (Borussia Dortmund), Conor Gallagher (Crystal Palace, on loan from Chelsea), Mason Mount (Chelsea), Kalvin Phillips (Leeds), Declan Rice (West Ham), James Ward-Prowse (Southampton).

MAFOWADI: Tammy Abraham (Roma), Jarrod Bowen (West Ham), Phil Foden (Man City), Jack Grealish (Man City), Harry Kane (Tottenham), Bukayo Saka (Arsenal), Raheem Sterling (Man City).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

KIKOLEZO: Sema ku-beat!

Moto waangamiza watoto 10 wachanga hospitalini Senegal

T L