Michezo

Kocha Kimanzi roho juu vijana wameiva Cecafa

December 5th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Francis Kimanzi amekariri kwamba vijana wake wa Harambee Stars wana kila sababu ya kuhifadhi taji la Cecafa walilolinyakua miaka miwili iliyopita mjini Machakos.

Mnamo 2017, Stars waliwapokeza Zanzibar kichapo cha 3-2 kupitia penalti, baada ya mchuano huo wa fainali kukamilika kwa sare ya 2-2 katika kipindi cha kawaida na cha zaida.

Kulingana na Kimanzi, kinachomwaminisha zaidi ni ukubwa wa kiwango cha hamasa miongoni mwa wachezaji wote 26 aliowaita kambini kujifua kwa kivumbi hicho.

“Tunatarajia kutia fora nchini Uganda na kurejea nyumbani na ufalme wa Cecafa 2019. Kila mchezaji aliyeitwa kambini anatawaliwa na motisha ya kutuvunia ushindi,” akasema Kimanzi katika kauli iliyosisitizwa na kiungo matata wa AFC Leopards, Wyvonne Isuza.

Makala ya 40 ya fainali za kuwania ubingwa wa Cecafa yataanza rasmi mjini Jinja wikendi hii, katika mchuano utakaoshuhudia wenyeji Uganda wakichuana na Ethiopia kabla ya Burundi kuvaana na Eritrea. Hata hivyo, Ethiopia wametishia kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho kutokana na ukosefu wa fedha.

Stars ambao wamepangwa na Tanzania, Djibouti na Zanzibar katika Kundi C, watapepetana na Djibouti siku ya Jumapili kabla ya kulimana na Tanzania na kisha Zanzibar mnamo Disemba 8 na 10 mtawalia.

Mbali na wenyeji Uganda, wapinzani wengine wanaotazamiwa kuwapa Stars ushindani mkali ni Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Uganda wako pamoja na Burundi na Eritrea katika Kundi A, huku DRC, Sudan, Sudan Kusini na Somalia wakikamilisha Kundi B.

Timu mbili za kwanza kutoka makundi yote matatu, pamoja na timu mbili zitakazomaliza mechi za makundi katika nafasi ya tatu zikiwa na alama nyingi zaidi, zitaingia hatua ya robo fainali.

Wakati huo huo, Nicholas Musonye ambaye ni Katibu Mkuu wa Cecafa, amesema bado wanatafuta wadhamini zaidi watakaofanikisha maandalizi ya fainali hizo. Kulingana naye, kila taifa linaloshiriki fainali za mwaka huu limetakiwa kutoa Sh2 milioni za usajili ambazo kiwango fulani kitatumika kuwatuza washindi.

“Tunatazamia kupata wafadhili zaidi kufikia Jumamosi kipenga cha kwanza kitakapopulizwa rasmi. Mwishoni mwa makala haya, tunatarajia kumtuza mshindi kitita kinono zaidi kuliko awali,” akasema Musonye.