Michezo

Kocha kumpigania chipukizi ambaye anatishiwa maisha

September 11th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Gareth Southgate amesisitiza kumpigania kiungo Declan Rice wa West Ham United baada ya mwanasoka huyo na familia yake kutishiwa maisha mitandaoni mara tu alipoamua kuchezea timu ya taifa ya Uingereza badala ya Jamhuri ya Ireland.

Rice ambaye aliichezea Ireland katika kiwango cha mechi za vijana, kabla ya kujiunga na timu ya watu wakubwa, na baadaye kuyoyomea Uingereza amekuwa akishambuliwa vikali kupitia kwa mitandao ya kijamii.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 20 ambaye ameichezea Uingereza ikiwemo mechi ya majuzi ambayo waliibuka na na ushindi 4-0 dhidi ya Bulgaria katika pambano la mchujo wa kufuzu kwa Euro 2020, alisema amepokea ujumbe wa kutishia maisha yake. Alisema kuna watu walioingia kwenye boma lake, huku akiongeza kwamba hata wazazi wake wamo hatarini.

“Nimepokea ujumbe kutoka kwa watu wanaodai wanapanga kunivamia nyumbani kupitia kwa mitandao wa jamii,” Rice alisema katika mahojiano na shirika la ITV News. Baada ya kunishambulia kupitia kwa jumbe hizo, sasa wameanza kutishia maisha ya wazazi wangu,” aliongeza.

Southgate alisema hata yeye ameshangazwa na vitisho hivyo dhidi ya Rice baada ya nyota huyo kuamua kuwa Muingereza.

“Nilihisi kwamba atakuwa mashakani baada ya kufanya uamuzi huo, na sasa anahitaji ulinzi wa kutosha hata kwa familia yake. Niliamua kutosema lolote wakati shughuli za kubadilisha uraia zilipokuwa zikiendelea kwa sababu nilitarajia vitisho vya aina hii. Hata hivyo, ningependa maafisa wa usalama wawe makini zaidi kuliko hapo awali.”

Sancho kushambulia

Southgate amefurahia ushirikiano wa Rice na viungo wengine wa kikosi chake, huku akifikiria kumpa Jadon Sancho nafasi kwenye safu ya ushambuliaji kushirikiana na Harry Kane badala ya Marcus Rashord ambaye ameonekana kulemewa katika mechi za majuzi.

Kutokana na tukio hilo, wachezaji wa kikosi hicho akiwemo Jordan Henderson wamemuunga mkono Rashford aliyetaka watu wajitambulishe wanapotumia jumbe zao kupitia kwa mitandao ya kijamii.

“Ni jambo la kushangaa watu kuruhusiwa kuanzisha mitandao na kuanza kutuma jumbe za kutishia wenzao maisha,” alisema kiungo huyo wa Liverpool.

“Nifikiriavyo, hivyo ni mojawapo wa njia za kukabiliana na watu wakorofi. Itakuwa vyema iwapo maombo yangu yatatiliwa mkazo,” alisema.

“Kwa wachezaji wenzangu, nawasihi wasisumbuliwe sana na propaganda za mitandaoni. Ni vyema kujumuika na mashabiki ambao wanatuunga mkono na kupuuza watu hatari kwa maisha yetu. Ni kawaifa watu wataendelea kutushutumu, lakini pia ni muhimu kuendelea na maisha yako ya kawaida. Hata sio lazima mtu asome maoni mitandaoni.”

Baada ya uingereza kushinda mechi zote tatu za mchujo wa kufuzu kwa Euro 2020, kocha Southagate anatarajiwa kuanza kubadilisha kikosi chake kwa mechi zijazo. Kikosi hicho kimejikusanyia jumla ya point nane baada ya kujibwaga uwanjani mara nne.