Michezo

Kocha Mauricio Pochettino sasa yuko huru kujiunga na klabu anayotaka

May 19th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Mauricio Pochettino sasa yuko huru kujiunga na klabu anayotaka bila vikwazo kutoka kwa waajiri wake wa zamani Tottenham Hotspur baada ya marufuku ya miezi sita yaliyomzuia kufanya hivyo kukamilika, vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti.

Pochettino, 48, amekuwa bila ajira tangu apigwe teke na Spurs mwezi Novemba 2019 kutokana na msururu wa matokeo duni.

Raia huyu wa Argentina, ambaye aliongoza Spurs kufika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya msimu 2018-2019, amehusishwa sana na klabu nyingine inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza, Newcastle United.

Miamba wa Uhispania Real Madrid pamoja na mabingwa wa zamani wa Italia AC Milan wamekuwa pia wakiaminika wanamezea mate Pochettino.

Tottenham ilizuia klabu yoyote kumnyakua kabla ya miezi sita kukamilika kwa kuweka sharti kuwa klabu inayomtaka lazima ilipe timu hiyo kutoka kaskazini mwa London Sh1.6 bilioni ndiposa imuajiri kwa sababu ilikuwa imelipa Pochettino fidia ya kumtema kabla ya kandarasi kutamatika.

Kukamilika kwa miezi hiyo sasa kunamweka Pochettino huru kuchukuliwa na klabu yoyote bila ya ada kutolewa kwa Tottenham.